Header Ads Widget

KUNDI LA KWANZA LA WAHAMIAJI LAWASILI RWANDA KUTOKA MAREKANI

 

Kundi la kwanza la wahamiaji saba waliorejeshwa kutoka Marekani limewasili Rwanda katikati ya Agosti, kati ya jumla ya 250 wanaotarajiwa kupokelewa chini ya makubaliano na utawala wa Rais Donald Trump.

Serikali ya Rwanda imesema wanne wataendelea kukaa nchini humo, huku watatu wakichagua kurejea makwao.

Mashirika ya haki za binadamu yameonya kuwa mpango huu unaweza kukiuka sheria za kimataifa endapo wahamiaji watarudishwa katika nchi ambako wanaweza kukumbwa na mateso au ukiukwaji wa haki. Hata hivyo, msemaji wa serikali Yolande Makolo amesema wahamiaji wote watapatiwa msaada na ulinzi unaohitajika na serikali ya Rwanda.

Wahamiaji hao wanahifadhiwa na shirika la kimataifa na wanatembelewa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) pamoja na huduma za kijamii za Rwanda.

IOM imethibitisha kuwa imewapokea ili kutathmini mahitaji yao ya msingi. Serikali ya Rwanda inasema inaendelea na makubaliano haya kwa kuwa karibu kila familia nchini humo imewahi kupitia machungu ya ukimbizi kufuatia historia ya mauaji ya kimbari ya miaka ya 1990.

Rwanda pia imewahi kupokea karibu wakimbizi 3,000 kutoka Libya kati ya mwaka 2019 na 2025 kupitia mpango wa UNHCR na Umoja wa Afrika. Rwanda ilikuwa na makubaliano kama hayo na Uingereza mwaka 2022, lakini mpango huo ulifutwa na serikali ya Labour mwaka 2024 licha ya kulipwa pauni milioni 240 na kujengewa makazi ya wakimbizi.

Haijulikani iwapo makubaliano ya sasa na Marekani yanahusisha malipo ya kifedha. Aidha, Rwanda imekuwa sehemu ya mazungumzo ya amani yanayosimamiwa Washington kuhusiana na mzozo wa muda mrefu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, japokuwa Kigali inakanusha kuhusika na kundi la waasi wa M23 linalopigana nchini humo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI