Fenerbahce imeachana na Jose Mourinho ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kujiunga na timu hiyo. Kuondoka kwa mreno huyo kumekuja siku mbili baada ya klabu hiyo ya Uturuki kuondolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na timu ya Benfica.
Taarifa ya klabu hiyo ilisema Mourinho "aliachana" na klabu hiyo, na kumshukuru mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 62 kwa juhudi zake.
"Tunamtakia mafanikio katika kazi yake ya baadaye," iliongeza taarifa hiyo.
Mourinho, ambaye amekuwa kocha wa vilabu 10 ikiwemo Chelsea, Manchester United na Tottenham, aliiongoza Fenerbahce kushika nafasi ya pili kwenye ligi kuu nchini Uturuki wakati wa msimu wake wa kwanza, lakini alikumbana na mizozo kadhaa.
Mabingwa Galatasaray walisema watamchuklia hatua za kisheria Mourinho, baada ya kumtuhumu kwa "kauli za kibaguzi" kwenye mchezo wa sare ya 0-0 wa mwezi Februari.
Mourinho alikanusha madai hayo, akisema yeye ni "sio mbaguzi, na akaifungulia kesi klabu hiyo akitaka kulipwa fidia ya £41,000.
Mourinho amekuwa mkosoaji wa mara kwa mara wa waamuzi nchini Uturuki, kwa sababu hiyo alipewa adhabu ya kufungiwa michezo minne, baadaye ikapunguzwa hadi miwili kutokana na maneno yake kuhusu waamuzi.
Alitoa maneno ya kutuhumu waamuzi baada ya mechi baina ya Fenerbahce dhidi ya Galatasaray msimu uliopita.
0 Comments