Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Hospitali ya mkoa Kigoma Maweni imesema kuwa upatikanaji wa damu kwa ajili ya wagonjwa wenye mahitaji imekuwa changamoto kubwa kutokana na kiasi kinachokusanywa kuwa hakitoshelezi mahitaji hivyo kuomba jamii ijitokeze kuchangia damu.
Mratibu wa damu salama mkoa Kigoma, Rajabu Mohamed alisema hayo wakati maafisa na watumishi wa jeshi la magereza mkoa Kigoma walipokuwa wakijitolea damu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kimkoa ya miaka 64 tangu kuanzishwa kwa jeshi la magereza.
Mohamed alisema kuwa wastani hospitali ya mkoa Kigoma Maweni imekuwa ikitumia Zaidi ya chupa 500 za damu kila mwezi kwa ajili ya Mama wajawazito, watoto, majeruhi wa ajali na wagonjwa wengine wanaohitaji damu hospitalini hapo ambapo amebainisha kuwa bado ukusanyaji damu unaofanyika haufikii mahitaji.
Kutokana na hali hiyo Mratibu huyo aliomba watu mbalimbali zikiwemo taasisi, mashirika, idara na watu binfasi kujitokeza kujitolea damu ili kuwezesha benki ya damu kuwa na akiba ya kutosha kwa ajili ya matumizi wakati wote badala ya kuanza kuomba inapotokea upungufu mkubwa.
Akizungumzia utoaji huo wa damu Mratibu Msaidizi wa Magereza mkoa Kigoma, Elizabeth Yohana alisema kuwa utoaji huo wa damu na kufanya usafi ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 64 ya jeshi hilo ambapo wao kama mkoa wameona wafanye shughuli hiyo.
Mratibu huyo wa magereza alisema kuwa wamewiwa kutoa damu baada ya kupata maombi mbalimbali kutoka taasisi hizo za afya na kwamba kwa huo mwanzo waliouonyesha wataendelea kujitolea Zaidi ili kuokoa watu wenye mahitaji.
Mwisho.
0 Comments