Na Matukio Daima Media ,Morogoro
MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewaomba wananchi wa Mkoa wa Morogoro na Watanzania kwa ujumla kumpa kura za ushindi wa kishindo pamoja na wagombea wa ubunge na udiwani ili kuendeleza kasi ya maendeleo ya taifa.
Akihutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Morogoro,Katika viwanja vya Tumbaku,Mkwawa Rais Samia alisema ushindi wa CCM ni msingi wa kuhakikisha miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa kote nchini inakamilika kwa wakati.
“Naomba kura zenu nyingi ili tuendelee kuwaletea maendeleo makubwa zaidi. Mkinipa wabunge na madiwani wa CCM, kazi itakuwa nyepesi na haraka zaidi, viongozi mkamsemee Mama, vikundi vya Hamasa mkamsemee Mama, wanafunzi wa vyuo vikuu na wengine mkamsemee Mama,mkamuombee kura” alisema.
Aliahidi kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa kuboresha vyanzo vilivyopo na kuanzisha vipya, kuimarisha sekta ya afya kupitia ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, majengo ya upasuaji na wodi za mama na mtoto, pamoja na kuhakikisha bima ya afya kwa wote.
Pia alisema Serikali ya CCM itaendelea kuwekeza kwenye sekta ya elimu, kusambaza umeme katika kila kaya, kuanzisha vituo vya kupooza umeme na kukuza matumizi ya nishati safi.
Kwa Mkoa wa Morogoro, Rais Samia alibainisha kuwa Serikali imejipanga kuufanya kuwa kitovu cha viwanda kwa kufufua viwanda vilivyokufa na kuanzisha vipya vikubwa, kujenga soko kubwa la machinga na wajasiriamali, kukuza kilimo kwa kujenga vituo maalum, kuendeleza barabara na kukuza utalii kwa kujenga kituo cha kisasa cha mikutano.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kupima maeneo na kutoa hati za kimila ili wananchi watumie ardhi kwa kilimo na biashara bila migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Katika hotuba hiyo, aliwatambulisha wagombea wa ubunge wa majimbo ya Mkoa wa Morogoro kwa tiketi ya CCM akiwataka wananchi wawape kura nyingi wao, madiwani na yeye kwa nafasi ya Urais ili kushirikiana naye kuendeleza kazi ya maendeleo.
Baadhi ya wagombea ubunge wa mkoa wa Morogoro akiwemo Abdulaziz Abood wa Morogoro Mjini, Denis Londo wa Mikumi, Zuberi Mfaume wa Morogoro Kusini, Hamis Taletale Morogoro Kusini Mashariki, Mecky Mdaku Ulanga, Salim Al Hasham Alaudin wa Ulanga, Dkt Rose Rwakatare wa Malinyi, Sarah Msafiri wa Ulanga, Abubakar Asenga wa Kilombero na Prof Paramagamba Kabudi wa Kilosa kwa nyakati wakazungumzia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika maeneo yao chini ya Uongozi wa Rais Samia ikiwemo katika sekta za afya, elimu, maji, miundo mbinu ya umeme, Reli, madaraja, barabara na maeneo mengine.
Wagombea hao kwa tiketi ya CCM wakawaomba wananchi kukipa ridhaa chama hicho tena kwa kuwachagua wagombea wake ili kukamilisha waliyoanzisha na kuanzisha miradi mipya ya maendeleo.
Mwisho.
0 Comments