Header Ads Widget

HASUNGA APETA, JIMBO LA MBOZI LACHELEWESHA MATOKEO HADI USIKU WA MANANE.


-Wapambe wakesha licha ya baridi kali.

Na Mwandishi Wetu, Mbozi.

 Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza matokeo ya kura za maoni kwa ajili ya kuwapata wagombea wa ubunge katika majimbo ya Mbozi na Vwawa, Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe.

Matokeo hayo yalitangazwa usiku wa manane wa Agosti 5, 2025, katika mazingira ya baridi kali, huku wajumbe na wafuasi wa wagombea wakikesha nje ya ukumbi wa CCM Mkoa uliopo mjini Vwawa wakisubiri hatima ya wagombea wao.

Kwa Jimbo la Mbozi, matokeo yaliyokuwa yakisubiriwa kwa hamu na msisimko mkubwa yalitangazwa na Saidi Ngondo, Msimamizi wa Uchaguzi wa Kura za Maoni ambaye pia ni Kiongozi wa Walimu Makada wa CCM Mkoa wa Songwe.
 Alimtangaza Mwalim, Onesmo Mkondya, kuwa ndiye mshindi kwa kupata kura 3,042, akimshinda kwa ushindani mkali Dkt. Siston Mgula, aliyepata kura 3,026 hivyo kufanya tofauti ya kura kuwa ni 16 pekee.
Wagombea wengine walioshiriki na kura walizopata kwenye mabano ni,
Philbert Mwampashi (617), Fredy Katoto (239),Rogers Mwamengo (197) na Frenk Ndile (178).

Katika Jimbo la Vwawa, ambapo hakukuwa na ushindani mkali sana, Japhet Hasunga alitangazwa mshindi na Msimamizi wa uchaguzi Halma Yusuph, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa.

Hasunga alipata kura 5,604, hatua inayomuwezesha kutetea nafasi yake.

Wagombea wengine wa Vwawa walioshiriki na kura walizopata kwenye mabano ni Tinkson Nzunda (1,451), Fanuel Mkisi (820), Geoffrey Mwashitete (392), Jumanne Sichizya (269) na 
Happy Mgalla (259) 

Kwa sasa, matokeo hayo yanasubiri uthibitisho na uteuzi wa mwisho kutoka ngazi ya juu ya chama, kabla ya wagombea walioteuliwa kutangazwa rasmi kwa ajili ya kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI