Hamid Ramadhan, MatukioDaima Media Dodoma
BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC)limeshauriwa kuimarisha elimu kwa wananchi hususani wanaoishi Vijijini ili kuongeza uelewa wa huduma hizo muhimu kupitia maonyesho ya Wakulima nanenane.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule,ameyasema hayo jijini Dodoma alipotembelea banda la Baraza hilo katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini.
Aidha Senyamule ,amesisitiza umuhimu wa Baraza hilo ni kuongeza kasi ya kutoa elimu ya matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira, ufuatiliaji wa bei za mafuta na huduma za maji na umeme, ili wananchi wa vijijini waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kilimo na biashara kwa tija zaidi
"Katika kuongeza ufanisi wa huduma hizo, nawaagiza wataalamu wa EWURA kutumia majukwaa hasa Jukwaa la Nanenane
Maonesho ya Nanenane, yanayofanyika kila mwaka, yamekuwa kiunganishi muhimu kati ya serikali, wakulima na wadau wa maendeleo,"Amesema
Awali,Mkuu huyo wa Mkoa amepokea maelezo kutoka kwa Afisa Uelimishaji na Uhamasishaji wa EWURA CCC, Lugiko Lugiko, kuhusu huduma zinazotolewa na Baraza hilo, ikiwemo kusikiliza na kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za mafuta, gesi, umeme na maji hatua inayotajwa kuwa ni chachu ya kuongeza ufanisi na uwazi katika sekta hizo.
Lugiko ameeleza kuwa ushiriki wa EWURA CCC katika Maonesho ya Wakulima mwaka huu ni sehemu ya mkakati wa kusogeza huduma kwa wananchi, hususani wale wa maeneo ya pembezoni, ambao mara nyingi hukosa taarifa sahihi na mwongozo wa namna bora ya kushughulikia changamoto na malalamiko yanayohusiana na huduma za nishati na maji.
0 Comments