Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema kuwa endapo kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi, kitaweka kipaumbele kwenye haki na usawa kwa kila Mtanzania.
Kauli hiyo imetolewa na mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Gombo Samandito Gombo, mara baada ya kukabidhiwa fomu ya kuwania urais na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele.
Akizungumza na waandishi wa habari, Gombo amesema kuwa ajenda yao kuu ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki yake stahiki, hasa katika maeneo ya afya na elimu.
Amesema kuwa kwa sasa kuna tofauti kubwa kati ya wananchi wenye uwezo na wale wasiokuwa na uwezo, jambo linalosababisha baadhi ya watu kupata huduma bora huku wengine wakiachwa nyuma.
Ameeleza kuwa huduma za afya na elimu bora hazipaswi kuwa kwa watu wachache bali ni haki ya kila Mtanzania, na kwamba serikali ya CUF inalenga kuhakikisha keki ya taifa inagawanywa kwa usawa ili kila mmoja anufaike nayo.
Mgombea huyo ameambatana na mgombea mwenza wake, Husna Mohamed Abdalla, katika tukio hilo, akisisitiza kuwa chama chao kitaendelea kusimamia misingi ya haki na usawa katika kila sekta ya maendeleo ya taifa.
Kwa mujibu wa CUF, mabadiliko ya kweli hayawezi kupatikana bila kuweka haki mbele, na hivyo wanawaomba Watanzania kuwapa nafasi ya kuongoza ili kutekeleza ajenda hiyo muhimu kwa mustakabali wa taifa.
0 Comments