Header Ads Widget

WAZIRI PINDI CHANA,REBECCA NSEMWA WAIBUKA KIDEDEA UBUNGE VITI MAALUM UWT MKOA WA NJOMBE,NEEMA MGAYA ANGUKA

 

Na Matukio Daima Media – Njombe

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana, ameibuka mshindi katika kinyang'anyiro cha nafasi ya Ubunge wa Viti Maalum kupitia Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Njombe kwa kupata kura 700 kati ya kura halali 841 zilizopigwa.

Ushindi huo unamuwezesha Dkt. Pindi Chana kuendelea kuiwakilisha Njombe katika nafasi ya Ubunge wa Viti Maalum kwa kipindi kingine cha miaka mitano, akitumia uzoefu wake wa kiuongozi na kisiasa kuendelea kuwahudumia wananchi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.

Katika mchuano huo mkali uliohusisha wanawake kadhaa wenye uzoefu na ushawishi mkubwa kisiasa, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Bi. Rebecca Nsemwa, alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 588. Rebecca ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za kiuongozi katika serikali, aliingia katika kinyang'anyiro hicho akiwa na rekodi nzuri ya utendaji aliouonesha alipokuwa DC, jambo lililompa ushindani mkubwa dhidi ya wanasiasa wenzake.

Nafasi ya tatu ilikwenda kwa aliyewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Njombe, Bi. Neema Mgaya, ambaye alipata jumla ya kura 263. Pamoja na kuwa na uzoefu wa ubunge, Neema hakuweza kuwashawishi wapiga kura wengi kurejesha imani kwake katika awamu hii.

Mshiriki mwingine, Anna Mwalongo, alipata kura 53 na kushika nafasi ya nne katika matokeo hayo. Wengine walioshiriki ni Scholastika Kivela aliyepata kura 47, Tegemea Mbogela kura 22, Magreth Kyando kura 5, na Tulalumba Mloge aliyepata kura 3 pekee.

Jumla ya kura zilizopigwa zilikuwa 841, ambapo kura moja ilihesabika kuwa imeharibika.

Ushindi wa Dkt. Pindi Chana umeonyesha namna ambavyo bado anaungwa mkono na wanawake wa CCM mkoani Njombe kutokana na mchango wake mkubwa katika uongozi wa kisiasa na maendeleo ya jamii. Dkt. Chana ambaye pia ni mwanadiplomasia, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za juu serikalini ikiwemo kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, na sasa akiwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

Wanachama wa UWT mkoani Njombe wameeleza matumaini yao kuwa kwa ushindi huo, Dkt. Pindi ataendelea kuwa kiunganishi madhubuti wa wanawake na serikali katika kuibua fursa za maendeleo na kusukuma mbele ajenda ya usawa wa kijinsia.

Zoezi la upigaji kura lilifanyika kwa amani na utulivu, huku wajumbe wakiendelea kuonesha mshikamano mkubwa ndani ya chama katika mchakato wa kuwapata wawakilishi bora kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI