WAZIRI wa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi Maalum Dk.Doroth Gwajima amewataka wanafunzi wasichana waliohitimu mafunzo ya uanagenzi kutoka Chuo cha ufundi Stadi (VETA) kutumia ujuzi wao kuanzisha shughuli za kiuchumi badala ya kukimbilia kwenye mahusiano na wanaume na kuwa tegemezi.
Waziri Gwajima alisema hayo katika mahafali ya kwanza ya wanafunzi 112 waliorasimisha ujuzi wao na wanafunzi 45 wanasomea ujenzi wa madaraja ya mawe wanaosomeshwa na Shirika la Ushirikiano wa kimataifa la serikali ya Ubelgiji (ENABEL) kupitia mradi wa Wezesha Binti ili kuwafanya ujuzi walionao utambulike rasmi na mamlaka mbalimbali.
Akizungumza na wanafunzi hao na wanajumuia wa Chuo Cha VETA Kigoma Waziri Gwajima alisema kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau imeona namna ya kuwasaidia wanafunzi wasichana wenye ujuzi lakini ujuzi wao hautambuliki ambapo kuingia chuo na kutoka na vyeti ambapo itawasaidia kupata ajira lakini kujiajiri kama wataalam na kuajiri vijana wenzao.
Waziri huyo wa maendeleo ya jamii alisema kuwa ujuzi waliopata wanafunzi hao ni jambo kubwa katika maisha yao kuliko kuanza kuingia kwenye mahusiano ambayo yatawaingiza kwenye vitendo vya ukatili hasa wanapokuwa hawana shughuli ya kuingiza kipato cha familia na kuanza kumtegemea mwanaume kwa kila kitu huku wakiwa na ujuzi ambao hawautumii inavyopaswa.
Akizungumza katika mahafali hayo Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Enabel Koenrad Goekint alisema kuwa Shirika hilo limewekeza kiasi cha Zaidi ya shilingi Bilioni tatu katika mradi huo ili kuwezesha wasichana wenye umri wa kati ya miaka 17 hadi 28 kupata ujuzi katika vyuo vya ufundi stadi mkoani Kigoma ambapo vijana 2300 watanufaika na program hiyo.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha wasichana hao kuendana na soko la ajira kwa kuajiriwa au kujiajiri kwa kupata mikopo na uwezeshaji kutoka taasisi za fedha.
Baadhi ya wanafunzi waliomaliza mafunzo chuoni hapo akiwemo Dotto Ramadhani walisema kuwa kauli ya Waziri Gwajima kuwataka kutojiingiza kwenye suala la mapenzi badala yake watafute shughuli za kuwaingizia kipati walisema kuwa watalizingatia hilo kwani linaweza kuwasaidia kwa maisha yao.
0 Comments