Header Ads Widget

CCM YATANGAZA MAJINA YA WAGOMBEA WA UBUNGE ,MAKALLA MCHAKATO UMEVUBJA REKODI

 


Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media  Dodoma

Baada ya kusubiriwa kwa hamu kwa muda mrefu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) hatimaye kimetangaza rasmi majina ya wagombea waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Tangazo hilo limetolewa leo na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla, katika Makao Makuu ya chama hicho jijini Dodoma.

Makalla amesema kuwa kazi ya kuchambua na kupitisha majina ya wagombea ilikuwa kubwa kutokana na idadi kubwa ya waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali. 

Amesema Kamati Kuu ya CCM ilifanya kazi hiyo kwa umakini na weledi ili kuhakikisha kila jina lililopitishwa linaakisi maadili, uwezo na utekelezaji wa sera za chama.


“Wagombea walikuwa wengi sana, kazi ya kuandaa orodha haikuwa nyepesi. Tulihakikisha tunamaliza kwa usahihi mkubwa, kwa kuzingatia maoni na mapendekezo ya vikao halali vya chama,” alisema Makalla.

Makalla aliwapongeza waombaji wote kwa kujitokeza kwa wingi mwaka huu, akibainisha kuwa mchakato wa mwaka huu umevunja rekodi kwa idadi ya wagombea. 

Aidha, alitoa shukrani kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwaongoza na kuwawezesha wajumbe kushiriki vikao mbalimbali, ikiwemo vile vya kimtandao vilivyolenga kufanya marekebisho ya katiba ya chama na kutoa mwongozo wa mchakato wa uteuzi.

“Tunamshukuru sana Mwenyekiti wetu kwa kutuongoza kwa hekima na uthabiti. Pia tunaishukuru Kamati Kuu kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa uadilifu na mshikamano,” aliongeza.

Makalla aliwahimiza wagombea wote ambao majina yao hayakupitishwa kutojiona kushindwa, bali waendelee kuwa na moyo wa kujitolea na kushiriki katika shughuli za chama. Alisisitiza kuwa CCM ina nafasi mbalimbali za uongozi na utumishi ambazo zinahitaji ushiriki wao.

“Tunawakaribisha kuendelea kuwa sehemu ya harakati za chama. Kutopitishwa leo si mwisho wa safari,” alisema.

Katibu huyo wa NEC pia alisema kuwa idadi kubwa ya wagombea ni ishara kwamba CCM kinaendelea kukubalika miongoni mwa wananchi na kina wanachama wengi barani Afrika, hali inayodhihirisha uimara wake kisiasa.

Kwa Jimbo la Dodoma Mjini, waliochaguliwa ni Eng Rashid Mashaka, Pascal Inyasi Chinyele, Samweli Malecela, Samwel Marwa Kisaro, Fatuma Yusufu Waziri, Robert Daniel Mwinje, Rosemary Chambe Jairo na Abdulhabib Jaffar Mwanyemba


Kwa upande wa Jimbo la Mtumba, majina yaliyopitishwa ni Anthony Peter Mavunde, Mussa Andrew Luhamo na Anthony Zacharia Kanyama

Makalla alisema kuwa idadi kubwa ya wagombea waliojitokeza ni ishara ya uhai wa chama na kuonyesha kuwa CCM inaendelea kukubalika kwa kiwango kikubwa miongoni mwa Watanzania. Aliongeza kuwa zaidi ya watu elfu tano waliomba kugombea ubunge, huku nafasi za udiwani zikivutia waombaji zaidi ya elfu thelathini

Hata hivyo, mchakato huo pia umefungua milango kwa sura mpya ambapo watu maarufu wakiwemo wasanii na wanahabari wamepata nafasi ya kugombea huku baadhi ya vigogo wakitupiliwa mbali 

Aidha Wanahabari Salim Kikeke amepitishwa kugombea Jimbo la Moshi Vijijini, msanii Baba Levo na mwanahabari Baruan Mhuza wamepata nafasi ya kugombea katika Jimbo la Kigoma Mjini, hatua iliyopokelewa kwa hisia mpya za matumaini kwa vijana na wadau wa sekta za sanaa na habari.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI