Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum Doroth Gwajima amewataka watanzania kutokubali ulaghai wa waganga wa kienyeji wasio na usajili ambao wamekuwa chanzo cha vitendo vya ukatili kwa kutoa tiba zinazochochea vitendo vya ulawiti na ubakaji.
Waziri Gwajima alisema hayo mkoani Kigoma akizundua kampeni ya kupambana na vitendo vya ukatili inayojulikana kama Badilika Tokomeza Ukatili inayoendeshwa kwa uratibu wa Shirika la Mpango wa maendeleo la serikali ya Ubelgiji (ENABEL) kupitia mradi wa wezesha Binti.
Alisema kuwa maelekezo ya waganga wa kienyeji wanaotoa kwa wateja wao ya kuwataka kuwabaka watoto wadogo, wazee au watu wa makundi maalum ili wapate utajiri au vyeo hayana uhalisia hivyo kutoa wito kwa watanzania kuwakataa waganga hao lakini pia kushirikiana na serikali katika kupiga vita utakiti wa kijinsia kwa namna yeyote.
Katika kuunga mkono kampeni hiyo Waziri Gwajima alisema kuwa serikali imefanya kazi kubwa kupitia wizara hiyo kwa kuja na sera na sheria ambazo zimekuwa na mafanikio makubwa kupunguza vitendo vya ukatili, ulawiti na ubakaji ingawa yapo maeneo hali bado siyo nzuri na kwamba wadau wamekuwa na mchango mkubwa kwenye kufanikisha kampeni hizo.
Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum Doroth Gwajima akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya kupinga ukatili inayoendeshwa na Shirika la ENABEL Mkoani Kigoma
Akizungumza katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mkazi wa ENABEL nchini, Koen GoeKint alisema kuwa kampeni hiyo imelenga kufikia watu 450,000 kufikia mwaka 2027 watakaoongozwa na manamabadiliko 150,000 ambao wataungana na serikali na wadau katika kuleta mabadiliko ya kijamii kupinga vitendo vya ukatili.Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la ENABEL, Koen Geokint akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa Badilika Tokomeza Ukatili
Geokint alisema kuwa mila,desturi na tamaduni potofu zimekuwa chanzo cha vitendo vya ukatili kwenye jamii na kwamba mambo hayo yanaweza kusimamiwa na kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii ambayo yataifanya jamii kuishi kwa Amani na usalama bila kuwepo kwa vitendo vya ukatili.
0 Comments