Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WATU wanaoaminika kuwa majambazi wamevamia basi la abiria lililokuwa linatoka Kigoma kuelekea Mwanza ambapo wamepora vitu mbalimbali vya abiria ndani ya basi hilo na kujeruhiwa abiria wanne kwa marungu.
Kamanda wa Polisi mkoa Kigoma,Filemon Makungu akizungumza na waandishi wa habari alisema kuwa tukio hilo limetokea julai 11 mwaka huu majira ya saa nne usiku kilometa mbili kutoka geti la kuingia kambi ya wakimbizi wa Burundi ya Nduta na kabla ya kufika kijiji cha Maloregwa wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.
Kamanda Makungu akizungumza kutoka wilayani Kibondo ambako alikwenda baada ya kupata taarifa za utekaji huo alisema kuwa watu wanne ambao walikuwa abiria kwenye basi la kampuni ya Adventure walijeruhiwa kwa marungu ambapo walipelekwa hospitali ya wilaya Kibondo kwa matibabu na kuruhusiwa.
Akieleza kuhusu uvamizi huo Kamanda Makungu alisema kuwa awali majambazi hao waliteka gari ndogo aina ya Toyota Kluger lililokuwa likitoka Kigoma likielekea Mwanza likiwa na mgonjwa ambaye alikuwa akipelekwa hospitali ya rufaa Bugando kwa matibabu.
“baada ya gari ndogo kusimamishwa bila ubishi walisimama na majambazi hao walispora mizigo na baadhi ya simu za abiria ambapo wakati wakiendelea na zoezi hilo lilitokea basi la Adventure ambalo lililoposimamishwa dereva alikaidi lakini ambapo mbele kidogo lilivamia mawe yaliyokuwa yamepangwa baraabara ambayo yalisababisha matairi kupasuka na gari hilo kulazimika kusimama,”alisema Kamanda Makung.
Alibainisha kuwa baada ya basi la abiria kusimama majambazi hao waliingi ndaani ya basi hilo na kuanza kupora simu, pesa na baadhi ya mizigo ya abiria na ndipo ikatokea kuwashambulia abiria hao wanne kwa marungu na kuwajeruhi.
Wakati majambazi wakiendelea na zoezi hilo polisi kutoka kambi ya wakimbizi Nduta wilayani Kibondo walipata taarifa na kufika eneo la tukio hivyo kuanza kurushiana risasi na majambazi hao ambao walikimbilia msituni.
Kamanda huyo wa polisi mkoa Kigoma alisema kuwa baada ya taarifa hizo alikwenda Kibondo usiku huo na zoezi la kuwasaka majambazi hao kwenye mapori linaendelea na kwamba atatoa taarifa rasmi ya tukio hilo baadaye.
Uvamizi huo wa majambazi hao unakuja siku tatu baada ya Mkuu wa mkoa Kigoma,Balozi Simon Sirro kuwafanya ziara wilayani humo ambapo pamoja na mambo mengine hatasita kuwashughulikia majambazi na watu wote watakaojihusisha na vitendo vya uhalifu mkoani Kigoma.
0 Comments