Header Ads Widget

BALOZI WA TANZANIA NCHINI CUBA HUMPHREY POLE POLE RASMI AJIUZULU NAFASI YAKE YA UBALOZI


 Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, amejiuzulu rasmi nafasi yake ya ubalozi na kuachana na uongozi wa umma, akitoa madai ya kuwepo na uvunjifu wa misingi ya haki, maadili, uwajibikaji na mwelekeo wa kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi CCM na serikali kwa ujumla.

Kupitia barua yake ya wazi aliyomwandikia Rais Samia Suluhu Hassan Julai 13, 2025, Polepole ameeleza kuwa hawezi kuendelea kuwa sehemu ya uongozi unaotanguliza maslahi binafsi badala ya ya wananchi.

Balozi Polepole, ambaye pia alikuwa Mkuu wa Kituo cha Uwakiilishi cha Tanzania nchini Cuba na mwakilishi wa Tanzania katika nchi rafiki za Karibe, Amerika ya Kati na baadhi ya mataifa ya Kusini mwa Amerika, amechukua hatua hiyo kwa kile alichokiita “tafakari ya kina kuhusu mwenendo wa uongozi wa sasa.”

Katika barua hiyo, Polepole ameeleza kuwa amefikia uamuzi huo kwa hiari, baada ya kuona kuwa misingi ya utawala bora, haki, maadili, uwajibikaji na maslahi ya wananchi havitiliwi tena mkazo serikalini wala ndani ya CCM. 

“Nimeamua kwa hiari yangu kujiuzulu nafasi yangu ya Uongozi wa Umma nikiwa Balozi baada ya kutafakari kwa kina juu ya mwenendo wa uongozi katika nchi yetu,” ameandika Polepole

“Kudhoofika kwa utekelezaji wa majukumu kwa misingi ya serikali kwa ajili ya ustawi wa wananchi kunanifanya nijitathmini mara kwa mara,”

‎Pia amedai kuwa kauli maarufu ya CCM inayosema Chama kwanza, mtu baadaye imepoteza maana, hasa pale inapogeuzwa kuwa kisingizio cha kuwakandamiza watu au kuhalalisha maamuzi yasiyo na maslahi ya wananchi.

“Nimejiuliza mara kadhaa, ni maslahi ya nani yanapangwa mbele, mtu, kikundi au chama taasisi?”

‎Humphrey Polepole aliwahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, akawa mmoja wa watu wa karibu wa Hayati Dkt. John Magufuli, kisha akachaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Novemba 2020 hadi Machi 2022.

Baada ya hapo, aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi, kisha kuhamishiwa Cuba ambako amehudumu hadi alipojiuzulu.

‎Ingawa amejivua nafasi ya serikali na utumishi wa umma, Polepole ameeleza kuwa bado atabaki kuwa mwanachama wa kawaida wa CCM na ataendelea kuwa mzalendo katika taifa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI