Watu saba wakiwemo wafanyabiashara wa nyama mjini Morogoro na wengi wao wakiwa ni wakazi wa Mkundi wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kufanya mauaji ya kikatili ya mfanyabiashara mwenzao Bernad Masaka, mkazi wa Mkundi, ambaye mwili wake ulikutwa umetupwa kijiji cha Manga, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama amesema watuhumiwa hao waliokamatwa ni Stanley Ng’ambi maarufu Jaha (31), Japhet Michael (29), Yusuph Mkamba (27), Nickson Ibrahim (43), Robson Rite (47), na Ernest Charles maarufu Chief (37), wote wakiwa na makazi Morogoro na Dar es Salaam.
Mmoja wa wafanyabiashara waliokamatwa , Stanley anadaiwa kumrubuni mfanyabiashara huyo kwenda eneo la Makunganya kufuata ng'ombe na badala yake wakamuua na kwenda kuutupa mwili wake Mkoani Tanga ambapo ulizikwa na halmashauri kwa kukosa ndugu baada ya kuokotwa, lakini upelekezi wa Polisi na vyombo vingine vya kiusalama, na baada ya kuwabana watuhumiwa, walifanikisha kufika eneo la tukio na kuufukua mwili huo na kuuchukua.
Inadaiwa kuwa mnamo Juni 1, 2025, marehemu alitekwa na kuuawa kwa kutumia vitu vyenye ncha kali baada ya kulaghaiwa kuwa anapelekwa Makunganya kununua ng’ombe. Baadaye mwili wake ulipelekwa na kutupwa mkoani Tanga.
Kamanda Mkama amesema uchunguzi wa awali unaonyesha tukio hilo lilitokana na wivu wa kibiashara.
Mwandishi wa matukio Daima alifika usiku Julai 02 mwaka huu,nyumbani kwa marehemu eneo la Mkundi na kushuhudia waombolezaji wakiwa wamekusanyika huku mwili wa marehemu ukiwa umehifadhiwa ndani ya basi dogo aina ya Costa.
Hata hivyo, waombolezaji na ndugu waligoma kuzungumza na vyombo vya habari.
Mwili huo uliondolewa majira ya saa 2.49 usiku kwenda Matumbulu, mkoani Dodoma kwa taratibu zaidi za maziko.
Wafanyabiashara wenzake wamesema kwa tahadhari kuwa Bernad alikuwa mtu wa nidhamu, aliyejitolea kulinda maslahi ya biashara halali ya nyama sokoni.
“Alikuwa zaidi ya askari polisi, alikuwa na uthubutu wa kusimamia uadilifu sokoni,” alisema mmoja wao.
Taarifa za ndani zinadai dereva mmoja aliyehusika na usafirishaji wa marehemu ndiye aliyefichua siri ya mauaji hayo baada ya kukamatwa na Polisi, ingawa alikataa kuelekeza eneo halisi la kutupwa mwili kwa madai aliyekwenda kuutupa mwili alikuwa bosi wake baada ya yeye kukataa na kulitelekeza gari.
0 Comments