Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Amos Makalla Makalla amesema Mwenyekiti wa CCM Dk Samia Suluhu Hassan amevitaka vikao vya uchujaji vitende haki visionee watu na haki ionekane ikitendeka na kuwaomba wanachama kuwa watulivu wakati wa mchakato wa uteuzi ndani ya chama.
Makalla ameeleza hayo leo Julai 3 wakati akizungumza na waandishinwa habari juu ya mchakato wa mchujo wa ndani ya chama unaofuata baada ya zoezi la uchukuaji fomu kuhitimishwa.
“Nimeelekezwa kwa niaba ya Halmashauri Kuu ya Taifa Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi Dk Samia Suluhu Hassan anavitaka vikao vya uchujaji vitende haki visionee watu, vitende haki na haki ionekane ikitendeka,” amesema Makalla.
Akieleza kuhusu ratiba ya ndani ya chama katika mchakato huo wa mchujo Makalla amesema kuwa kuanzia kesho Julai 4 mwaka huu wanaanza vikao vya kamati za siasa katika Kata kwa ajili ya uchujaji na kutoa mapendekezo ya wagombea wa madiwani na viti maalumu.
Amesema Julai 9, kamati ya siasa mkoa kufanya uteuzi wa mwisho wa nafasi za udiwani na Julai 19, kamati kuu ya CCM itafanya uteuzi wa mwisho wa wabunge na wawakilishi.
Makalla amesisitiza CCM inajipambanua katika kupambana na kudhibiti rushwa na ndiyo sababu wameongeza wajumbe katika mchakato wa uchujaji ili kupambana na vitendo vya rushwa katika kura za maoni, hivyo wagombea watakaoshiriki katika vitendo vya rushwa watakuwa wamejiondoa kwenye mchakato.
0 Comments