Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabir Omari Makame, ametoa onyo kali kwa vijana wanaojihusisha kimapenzi na watoto wa kike, akisisitiza kuwa wasichana hao ni "nyara za serikali" na jamii inapaswa kuwalinda kwa nguvu zote.
Makame alitoa kauli hiyo Julai 23, 2025, wakati akiwahutubia wananchi wa Isongole, Wilaya ya Ileje, kwenye mkutano wa hadhara ikiwa ni muendwlezo wa ziara zake za kutembelea Halmashauri zote za Mkoa huo kwa lengo la kujitambulisha, kusikiliza na kutatua kero mbalimbali.
“Tunayo changamoto kubwa ya mimba za utotoni katika mkoa wetu, jambo linalohatarisha mustakabali wa watoto wetu wa kike hivyo ni jukumu letu kama viongozi na jamii kwa ujumla kuwasimamia watoto hawa wamalize elimu yao".
"Lazima tuchukue hatua kwa vijana wote wanaocheza na watoto wa kike,” alisema Makame kwa msisitizo.
Akieleza umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike, Mkuu huyo wa Mkoa alitumia mifano ya viongozi wanawake walioko madarakani kama ushahidi wa mafanikio yanayotokana na elimu.
“Leo hii tunaye Mkuu wa Wilaya hapa ni mwanamke, na Mkurugenzi pia ni mwanamkehivyo kama wangeachishwa masomo yao kwa sababu ya mimba za utotoni, tungekuwa tumepoteza viongozi hawa wa mfano,” aliongeza.
Makame aliwasisitiza vijana wanaojihusisha kimapenzi na watoto wa kike kuacha mara moja tabia hiyo kwani mbali na kukwamisha ndoto za watoto wa kike, lakini zitawaweka kwenye misukosuko.
0 Comments