Header Ads Widget

WANARIADHA FILBERT BAYI SEKONDARI WAPEWA FEDHA USHINDI UMISSETA.


Na Mwandishi Wetu, Kibaha Matukio Daima App

SHULE ya Sekondari ya Filbert Bayi imetoa zawadi ya fedha taslimu kwa timu ya riadha ya shule hiyo iliyofanya vizuri kwenye mashindano ya Umoja wa Michezo Shule za Sekondari na Taaluma (UMISSETA) Taifa iliyomalizika hivi karibuni Mkoani Iringa.

Akikabidhi fedha hizo kwa wanamichezo tisa shuleni hapo, Ofisa Elimu Mkoa wa Pwani Jimmy Nkwamu alisema kuwa kutokana na ushindi wa timu hiyo kumeufanya Mkoa huo kuwa washindi wa kwanza wa mchezo huo kitaifa na wanne kwa michezo yote.

Nkwamu alisema kuwa kilichofanya timu ya riadha kuwa ya kwanza ni maandalizi yaliyofanywa na Mkoa ambapo iliweka kambi ya muda mrefu pamoja na motisha iliyokuwa ikitolewa kila timu inapofanya vizuri pamoja na ushirikiano na mshikamano uliokuwepo baina ya viongozi wa Mkoa na wachezaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu na Mwenyekiti Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi za Filbert Bayi alisema kuwa lengo la kutoa zawadi hizo za fedha taslimu ni kuwahamasisha wachezaji waliofanya vyema ni kuwapa hamasa ili waendeleze vipaji na vipawa vyao kwenye mchezo huo.

Bayi alisema kuwa walitenga fedha kwa kila mshindi kwa mchezo huo kwa mbio zozote kiasi cha shilingi 50,000 kwa atakayeshinda medali ya dhahabu, fedha shilingi 30,000 na shaba ni shilingi 20,000 ambapo Sharifa Rashid alipata dhahabu tatu.

Naye ofisa michezo wa Mkoa wa Pwani Grace Bureta alisema kuwa shule hiyo ni moja ya shule ambazo zimekuwa zikiufanya mkoa huo kufanya vizuri kwenye michezo ya shule za sekondari nchini UMISSETA kwani ina mazingira mazuri ya kuwaandaa wachezaji.

Wachezaji wengine waliotunukiwa ni Wiliam Makaranga dhahabu moja, Samwel Samwel shaba moja , Emanuel Dotto fedha mbili, Salma Samwel fedha moja huku wengine wakishinda kwenye mbio za kupokezana vijiti ambao ni Kimana Sitta, Zainab Seleman, Lucia Nestor, Enos Manengelo ambapo Meshack Emanuel akishika nafasi ya tano kurusha kisahani na Rashid Mtindaji alikuwa wanne kuruka chini.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI