Na Adery Masta.
Katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba yanayoendelea Temeke Jijini Dar es Salaam, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imekuwa kivutio kikuu – si kwa mandhari ya banda lake tu, bali kwa bunifu zilizogusa maisha halisi ya Mtanzania wa kawaida.
DIT imeibuka kuwa kitovu cha ubunifu wa kitaifa, ikionesha wazi kuwa elimu ya vitendo ndiyo msingi wa maendeleo ya kweli.
Moja ya mambo yaliyovutia wengi kwenye banda la DIT ni mashine ya kutengeneza sabuni za kufulia , suluhisho rahisi kwa vikundi vya vijana na kina mama wanaojihusisha na ujasiriamali. Sambamba na hiyo, kulikuwepo pia mashine ya kukausha mbogamboga na dagaa hatua kubwa katika kuhifadhi mazao ya chakula kwa muda mrefu bila kemikali .
Hizi ni teknolojia zinazozalishwa ndani ya nchi, na ndizo zinazohitajika kuibadilisha Tanzania kutoka kuagiza hadi kuzalisha.
Aidha Kupitia DIT Company, kampuni tanzu ya taasisi hiyo, wageni walipata nafasi ya kuona bidhaa bora kabisa za ngozi zinazozalishwa kwa ubunifu wa hali ya juu — ikiwa ni pamoja na viatu vya ngozi , mikanda, na mipira. Ubora wake uliwashangaza wengi na kuthibitisha kuwa bidhaa bora hazitoki mbali zinatoka DIT, Kwasababu DIT kupitia kampasi yake ya Mwanza imekuwa kivutio kikubwa mno kwa watu wengi na hii imepewa kipaumbele na serikali kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaochagua kusoma kozi hizo za umahiri wa bidhaa za ngozi.
> “Viatu hivi ni vizuri kuliko vingine nilivyowahi kuona. Tanzania tunaweza!” – Mgeni wa banda
Kivutio kingine kilichogusa nyoyo za wengi ni Mama Track – mfumo wa kidigitali unaosaidia kufuatilia afya za kina mama wajawazito. Mfumo huu umetengenezwa na mwanafunzi wa DIT Penina Macha, akilenga kuleta suluhisho kwa changamoto zinazowakabili wajawazito vijijini na mijini.
Mfumo huu ni mfano wa namna DIT inavyowakuza wanafunzi kuwa wavumbuzi wa maisha halisi, si watahiniwa wa mitihani pekee.
Katika banda hilo hilo, DIT pia iliwasilisha bidhaa za asili kama mafuta ya kupaka ngozi, sabuni za usafi na bidhaa nyingine zinazotokana na mimea asilia. Zote zimetengenezwa kitaalamu kwa kutumia maarifa ya kisayansi na teknolojia ya kisasa kutoka ndani ya taasisi hiyo.
Moja ya vumbuzi zilizowashangaza wengi ni gari linalotumia gesi, mojawapo ya hatua za DIT katika kuelekea kwenye teknolojia rafiki kwa mazingira. Hili ni uthibitisho kuwa taasisi hii haibuni kwa ajili ya leo tu, bali kwa Tanzania ya kesho.
Mbali na mashine na bidhaa, DIT pia ilitoa elimu kwa umma juu ya shughuli zake za usanifu wa majengo, ikionesha michoro, miradi halisi na programu wanazotumia kukuza wataalamu wa sekta hiyo. Ni eneo muhimu sana hasa katika miji inayokua kama Dar es Salaam na Dodoma.
Banda la DIT lilijaa wageni kila siku. Baadhi yao waliongea nasi:
> “Hii ndiyo elimu tunayoihitaji. Elimu inayozalisha mashine na bidhaa zinazosaidia jamii.”
— Amina S., Mwalimu
> “Mama Track imenigusa sana. Nashukuru kwa kuona wanawake wakivumbua teknolojia kwa ajili ya wanawake.”
— Dkt. Flora M., Mtaalamu wa Afya
> “Hawa vijana wa DIT ni wa kushangiliwa. Tanzania ina hazina kubwa ya vipaji.”
— Joseph K., Mwekezaji wa Teknolojia
Kwa kile kilichooneshwa Sabasaba 2025, DIT haibaki nyuma. Taasisi hii inaonesha wazi kuwa teknolojia siyo ya mataifa ya mbali pekee — ni ya kila Mtanzania. Ni dhahiri kuwa DIT siyo tu chuo cha teknolojia, bali ni daraja kati ya elimu na maendeleo halisi ya taifa.
Ikiwa hukufika Sabasaba mwaka huu, usijali — teknolojia za DIT zinaendelea kuenea. Na kama kuna mahali pa kutazama kesho ya Tanzania ni katika Taasisi ya Teknolojia Dar Es salaam.
Yafuatayo ni matukio katika picha yaliyojili katika Banda la DIT Viwanja vya Saba Saba mwaka huu 👇👇👇
0 Comments