Na Thobias Mwanakatwe, MANYONI
WANANCHI wapatao 11,250 wa vijiji 10 katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida wataondokana na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kufuatia Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kujenga mradi wa maji ambao utakapokamilika utagharimu zaidi ya Sh.milioni 933.481.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Manyoni,Mhandisi Gabriel Ngongi,akitoa taarifa leo (Julai 24, 2025) kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi,amesema ujenzi wa mradi wa maji katika vijiji 10 uliibuliwa na wananchi mwaka 2022 na kuingizwa katika Programu ya Maji ya Visima 900 kwa hatua ya utekelezaji.
Mradi huo utavinufaisha vijiji vya Magasai,Solya,Mpapa,Chidudu,Mwitikila,Damwelu,Lulanga,Kazikazi,Kalangali,Mbugani pamoja na Shule ya Sekondari ya Wasichana Solya.
Amesema ujenzi wa mradi huu ulianza rasmi Januari 14, 2025 na unatarajia kukamilika Agosti 4, 2025 ambapo unasimamiwa na ofisi ya Meneja RUWASA Wilaya ya Manyoni kwa kushirikiana na ofisi ya Meneja wa RUWASA Mkoa wa Singida.
"Mradi huu unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi 933,481,509.50 kupitia fedha za Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF), hadi sasa jumla ya shilingi 664,686,371 .30 zimetolewa na kutumika," amesema Ngongi.
Ngongi amesema shughuli zilizotekelezwa hadi sasa ni kufanya utafiti na kuchimba visima vya maji katika vijiji 10,kununua na kufunga mfumo wa kusukuma maji unaotumia nishati ya jua katika vijiji 10,kununua na kufunga matenki ya plastiki ya ujazo wa lita 10,000 na kujenga vioski pamoja na mtandao wa bomba kwa ajili ya kutolea huduma ya maji kwa wananchi.
"Utekelezaji umefikia asilimia 80 ambapo jumla ya vijiji 8 vya Magasai, Solya, Mpapa, Chidudu,Mwitikila,Damwelu,Lulanga na Kazikazi, ujenzi umekamilika na wananchi wanapata huduma ya maji," amesema Ngongi.
Mhandisi Ngongi amesema matarajio ya mradi huu ni kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika vijiji 10 ambapo jumla ya wananchi 11,500 sawa na asilimia 2.7 ya wananchi wa Wilaya ya Manyoni wanaoishi vijijini watanufaika na huduma ya maji safi na salama kwa gharama nafuu ya shilingi 30 kwa ndoo moja ya lita 20.
"Mradi huu umesaidia kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi 8000 ndani ya mita 400 toka kwenye makazi yao hivyo kuwawezesha kuwa na muda wa kutosha kufanya shughuli za maendeleo na kuboresha afya zao,upatikanaji wa maji katika Shule ya Wasichana Solya na kutoa ajira za muda mfupi kwa wananchi 30," amesema Ngongi.
Ngongi ameongeza kuwa RUWASA kwa kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni imetoa elimu ya utunzaji wa vyanzo vya maji kwa kuhamasisha jamii kupanda miti ambayo ni rafiki wa vyanzo vya maji kuzunguka maeneo ya mradi.
Naye Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, ameipongeza RUWASA kwa jinsi ambavyo imekuwa ikitekeleza miradi ya maji kwa uadilifu na hivyo kuwaondolea wananchi changamoto ya upatikanaji wa maji vijijjni na miji.
"Zipo wizara nyingi hapa nchini lakini kiukweli Wizara ya Maji inafanya kazi vizuri na kwa uadilifu mkubwa, wizara hii inamheshikisha sana rais kwa kila mkoa,wilaya na halmashauri kuna miradi mingi ya maji imetekelezwa," amesema Ussi.
Ussi amesema tangu walipoanza mbio za Mwenge wa Uhuru ulipoanza mbio zake katika Mkoa wa Pwani kila wilaya na halmashauri wanayoitembelea kuna miradi mingi ya maji.
0 Comments