Header Ads Widget

UTEUZI WA MGOMBEA URAIS CCM 2025,POLE POLE AMEPOTOSHA -MASIGA


Na MASIGA GA 


Aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Ndugu Humphrey Polepole, amenukuliwa akidai kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakikufuata utaratibu wa kikatiba katika uteuzi wa mgombea wake wa urais kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Hata hivyo, uchambuzi wa kina wa Katiba ya CCM, toleo la mwaka 2025, unaonesha wazi kuwa kauli hizo hazina msingi wa kikatiba na zinapaswa kuchukuliwa kama upotoshaji unaolenga kuondoa umakini wa wanachama na wananchi ukiwa na msukumo wa maslahi binafsi. 


Katiba Ya CCM ndio Sheria Mama Inayotoa Mwelekeo



Ibara ya 99(1) ya Katiba ya CCM inatamka kuwa “Kutakuwa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa”, na Ibara ya 99(2) inaeleza kuwa, “Mkutano Mkuu wa CCM Taifa utakuwa ndicho kikao kikuu kupita vyote na ndicho kitakachokuwa na madaraka ya mwisho ndani ya CCM.”


Kwa mujibu wa ibara hii, ni wazi kuwa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ndicho chombo chenye mamlaka ya mwisho katika kufanya maamuzi yote makubwa ya chama, ikiwemo uteuzi wa mgombea urais.


*Ibara 100(5)(b): Mamlaka ya Kuteua Mgombea Urais*


Katiba hiyo hiyo ya CCM inasisitiza kupitia Ibara ya 101(5)(b) kwamba moja ya kazi mahsusi za Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ni:-


"Kuchagua jina moja la mwanachama atakayesimama katika uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM."


Kwa maana hiyo, Katiba haijatoa masharti kuhusu namna jina hilo linavyopaswa kufikishwa mbele ya Mkutano Mkuu. Haijataja kuwa ni lazima majina yapitishwe kwenye Sekretarieti, Kamati Kuu (CC), Kamati ya Maadili au hata Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC). Kinachoamuliwa na Mkutano Mkuu ndicho uamuzi wa mwisho wa chama.


*Muktadha wa Utamaduni vs Katiba*


Ndugu Polepole amedai kuwa jina la Dkt. Samia Suluhu Hassan lilipendekezwa na mjumbe mmoja tu katika Mkutano Mkuu, hivyo lilipaswa kupitia vikao vya awali vya chama. Hili ni dai linalopotosha kwa kuwa katika Katiba hakuna kifungu kinacholazimisha mchakato huo wa awali. Kinachotakiwa kikatiba ni kwamba jina lipitishwe na kupigiwa kura na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, jambo ambalo lilifanyika kwa mujibu wa taratibu.


Tunaelewa kuwa kwa miaka iliyopita, uteuzi wa wagombea wa nafasi hiyo ulitokana na mchakato wa awali kupitia vikao vya chini vya chama. Hata hivyo, huo ulikuwa ni utamaduni wa kisiasa na si amri ya kikatiba. Katika mazingira yoyote, Katiba inachukua nafasi ya juu zaidi ya utaratibu wa desturi au utamaduni.


*Uteuzi wa Dkt. Samia ni Halali, Kisheria na Kisiasa*


Mkutano Mkuu wa CCM Taifa mwaka 2025 ulifanya kazi yake kwa mujibu wa Katiba. Uteuzi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan ulipitishwa rasmi na Mkutano huo kwa mujibu wa Ibara ya 101(5)(b). Hakukuwa na uvunjaji wowote wa Katiba kama inavyodaiwa na Ndugu Polepole.

Kama Katiba inatamka kuwa Mkutano Mkuu una mamlaka ya mwisho, basi hakuna haja ya masharti ya ziada. Vikao vingine vya chini vya chama vinaweza kutoa mapendekezo, lakini uamuzi wa mwisho uko mikononi mwa Mkutano Mkuu.


Polepole Anajikanganya Katika Tafsiri ya Katiba

Ni jambo la kusikitisha kuwa Ndugu Polepole, ambaye aliwahi kushika nafasi nyeti ndani ya chama, anashindwa kufasiri Katiba ya CCM kwa usahihi au anapotosha makusudi kwa sababu za binafsi au ajenda za nje ya chama.

*#KaziNaUtuTunasongaMbele




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI