Uingereza italitambua taifa la Palestina mwezi Septemba endapo Israel haitachukua "hatua madhubuti za kukomesha hali ya kutisha inayoshuhudiwa Gaza," Waziri Mkuu Sir Keir Starmer amesema.
Starmer pia amesema Israel sharti ifikie matakwa mengine ikiwa ni pamoja na kukubali kusitishwa kwa mapigano, kujitolea kufikiwa kwa amani na utulivu wa muda mrefu ambayo inatoa suluhu ya mzozo wa nchi mbili, na kuruhusu Umoja wa Mataifa kurejelea upya usambazaji wa misaada, la sivyo Uingereza itachukua hatua dhidi yake kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Septemba.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema hatua hiyo "inatunza ugaidi wa kutisha wa Hamas".
Serikali ya Uingereza iliwahi kusema kutambuliwa kwa Palestina kunapaswa kuzingatiwa wakati kunaweza kuwa na athari kubwa, kama sehemu ya mchakato wa amani.
Hata hivyo Wazi Mkuu huyo amekuwa akishinikizwa na wabunge ikiwa ni pamoja na wale kutoka kwa chama chake kuchukua hatua hiyo haraka iwezekanavyo.
Wiki iliyopita Ufaransa pia ilitangaza kulitambua rasmi taifa la Palestina mwezi Septemba - taifa la kwanza la G7 la nchi tajiri zaidi duniani kufanya hivyo.
Katika taarifa kwa waandishi wa habari baada ya kufanya mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri, Sir Keir alisema anatangaza mpango huo kwa sababu ya "hali isiyovumilika" huko Gaza na wasiwasi kwamba "uwezekano wa kufikiwa kwa suluhisho la serikali mbili unapungua".
Aliwaambia waandishi wa habari kwamba lengo la Uingereza la kuwa na "Israel salama na taifa huru la Palestina" linakabiliwa na "shinikizo kubwa kuliko ilivyokuwa hapo awali".
Starmer pia aliongeza kuwa "lengo kuu" lilikuwa kuboresha hali katika eneo la Gaza, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba misaada inawafikia raia wanaokabiliwa na hali ngumu.
Akielezea hatua ambazo Uingereza ilitaka serikali ya Israel kuchukua, Sir Keir pia alisema inapaswa kuweka wazi hakutakuwa na mpango wa kugawanywa kwa eneo la katika Ukingo wa Magharibi.
Serikali ya sasa ya Israel inapinga mpango wa kuelekea suluhu ya mataifa mawili na kuna uwezekano mkubwa isikubali masharti hayo.
0 Comments