Ufaransa italitambua rasmi taifa la Palestina mnamo Septemba, Rais Emmanuel Macron ametangaza, na kulifanya kuwa taifa la kwanza la G7 kufanya hivyo.
Katika chapisho kwenye X, Macron alisema kuwa tamko rasmi litatolewa wakati wa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York.
"Haja ya dharura leo ni vita vya Gaza kumalizika na raia kuokolewa. Amani inawezekana. Tunahitaji kusitisha mapigano mara moja, kuachiliwa kwa mateka wote, na misaada kubwa ya kibinadamu kwa watu wa Gaza," aliandika.
Maafisa wa Palestina waliafiki uamuzi wa Macron, huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akisema hatua hiyo "inautunuku ugaidi" kufuatia shambulio la Hamas la 7 Oktoba 2023 nchini Israeli.
Marekani "inapinga vikali" tangazo la Macron, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio alisema, akielezea uamuzi huo kama "wa kutojali".
G7 ni kundi la mataifa makubwa yaliyoendelea kiviwanda ambayo, pamoja na Ufaransa, yanajumuisha Marekani, Uingereza, Italia, Ujerumani, Canada na Japan.
Israel haiitambui serikali ya Palestina, na serikali ya sasa ya Israel inapinga kuundwa kwa serikali ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi na Gaza, ikisema kuwa serikali kama hiyo itakuwa tishio kwa uwepo wa Israeli.
Waziri Mkuu Netanyahu aliandika katika chapisho kwenye X: "Serikali ya Palestina katika hali hizi itakuwa ufunguo wa uzinduzi wa kuangamiza Israeli - sio kuishi kwa amani kando yake. Wacha tuwe wazi: Wapalestina hawatafuti serikali pamoja na Israeli; wanatafuta taifa bila Israel."
Ni nani anaitambua Palestina kama taifa?
Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas (kushoto) na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wakati wa mazungumzo huko Paris mnamo Julai 2022
Hivi sasa,taifa la Palestina linatambuliwa na zaidi ya nchi 140 kati ya 193 wanachama wa UN, pamoja na wanachama wa Kundi la Kiarabu katika Umoja wa Mataifa, Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu, na Vuguvugu la Wasio na Msimamo.
Baadhi ya nchi za Ulaya ni miongoni mwao, ikiwa ni pamoja na Uhispania, Ireland, na Norway, ambazo zilitambua rasmi taifa la Palestina mnamo Mei 2024. Kabla ya hapo, ni nchi chache tu za Ulaya zilizofanya hivyo - nyingi zikiwa zimefanya hivyo mnamo 1988, wakati walikuwa sehemu ya kambi ya Soviet.
Hata hivyo, mfuasi mkuu wa Israeli, Marekani, na washirika wake - ikiwa ni pamoja na Uingereza na Australia - hawajatambua taifa la Palestina. Australia imeonyesha kuwa inaweza kufanya hivyo ili "kujenga kasi kuelekea suluhisho la mataifa mawili" linalosimamiwa na Israeli.
0 Comments