Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima. App DODOMA
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anamlingi Macha, amesema kuwa Mkoa wa Simiyu umeendelea kuwa kinara wa kitaifa katika uzalishaji wa zao la pamba, na sasa umechukua nafasi muhimu kimataifa kupitia kilimo cha pamba hai (organic cotton).
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 18 2025, jijini Dodoma Macha amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewezesha mkoa huo kuvuka matarajio kwa kuwekeza katika miundombinu, huduma za ugani na upatikanaji wa pembejeo bora kwa wakulima wa pamba.
“Kwa sasa zaidi ya asilimia 60 ya pamba yote nchini huzalishwa hapa Simiyu, na uzalishaji umeongezeka kutoka tani 64,594 mwaka 2020 hadi tani 140,000 mwaka 2024,” alisema Macha.
Aliongeza kuwa Simiyu ni mkoa pekee Tanzania unaolima pamba hai, na uzalishaji wake umeongezeka kutoka tani 10,300 msimu wa 2021/2022 hadi tani 12,285 msimu wa 2022/2023, hali iliyoufanya mkoa huo kushika nafasi ya saba duniani katika uzalishaji wa pamba hai, nyuma ya mataifa kama China, India, Uturuki na Tajikistan.
Aidha, Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu (SIMCU 2018 Ltd) kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), kimefanikiwa kufufua kiwanda cha kuchakata pamba cha Sola Ginnery kilichopo Wilaya ya Maswa kwa gharama ya shilingi bilioni 4.0.
“Kiwanda hiki kimeongeza thamani ya pamba kwa wakulima wetu, kimetoa ajira kwa vijana na kimepunguza gharama za usafirishaji wa mazao ya wakulima,” alieleza.
Mkoa pia umeendelea kuboresha huduma za ugani na kuwezesha wakulima kupitia maafisa ugani waliopatiwa vifaa vya kisasa, usambazaji wa pembejeo na mikopo midogo ya kilimo kutoka taasisi za fedha.
“Pamba ni zaidi ya zao ni uti wa mgongo wa uchumi wa wakazi wa Simiyu lakini pia tunaishukuru Serikali kwa kuwezesha mapinduzi haya,” amehitimisha Macha.
MWISHO.
0 Comments