Na Hamida Ramadhan,,Matukio Daima Media Dodoma
MWAKILISHI wa Mashujaa wa vita vya Kagera, Balozi Brigedia Jenerali mstaafu Francis Bernard Mndolwa, amewasihi Watanzania kuwa wazalendo kwa nchi yao, akisisitiza kuwa uzalendo ni silaha muhimu ya kulinda amani na mshikamano wa kitaifa.
Akizungumza katika tukio la kuwakumbuka mashujaa wa vita hivyo, Brigedia Jenerali Mndolwa alisema anajivunia kuwa sehemu ya waliopigania uhuru wa taifa, na kuwataka Watanzania wote wakiwemo wafanyakazi wa kada mbalimbali kutanguliza maslahi ya taifa mbele.
“Ninajivunia kuwa mmoja wa wapigania uhuru. Uzalendo si jukumu la jeshi pekee, ni wajibu wa kila Mtanzania, kila mfanyakazi Hata ninyi waandishi wa habari nawasihi muwe wazalendo kwa kuandika habari zinazowaheshimisha na kuwaelimisha Watanzania,” alisema.
Aliongeza kuwa taifa linaendelea kufurahia amani kwa sababu ya misingi imara ya umoja iliyowekwa na waasisi wa taifa, akiwataja Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume kama mifano ya viongozi waliotanguliza maslahi ya taifa.
“Kuna mataifa mengi duniani yaliyopoteza amani kwa kukosa uzalendo na mshikamano Tanzania tumeweza kudumu kwa amani kwa sababu ya msingi huo umoja kati ya Tanzania Bara na Visiwani ni jambo tunalopaswa kulilinda kwa nguvu zote,” alisema.
“Tusiige mwenendo wa mataifa mengine kama Urusi na China wanaopambana kwa maslahi yao Sisi tunahitaji mshikamano wa kweli Bara na Visiwani tushirikiane kuilinda amani yetu.”
Brigedia Jenerali Mndolwa alihitimisha kwa kuwataka Watanzania kuenzi kazi ya mashujaa kwa vitendo, hasa kwa kulinda amani, kushiriki maendeleo, na kudumisha umoja wa kitaifa.
0 Comments