London, Uingereza – Klabu ya Arsenal iko mbioni kukamilisha usajili wa mshambuliaji hatari wa kimataifa wa Sweden, Viktor Gyökeres, ambaye anatarajiwa kutua jijini London leo jioni kabla ya kufanyiwa vipimo vya afya kesho asubuhi.
Gyökeres, anayekipiga katika klabu ya Sporting CP ya Ureno, amekuwa katika rada ya Arsenal kwa miezi kadhaa sasa, na uongozi wa klabu hiyo ya Emirates umeharakisha dili hilo kufikia makubaliano ya dau linaloripotiwa kufikia pauni milioni 51 pamoja na nyongeza kulingana na mafanikio.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26, ambaye alifunga mabao 43 katika mashindano yote msimu uliopita, anatazamiwa kuwa sehemu muhimu ya safu ya ushambuliaji ya kocha Mikel Arteta, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya England.
Arsenal inatarajiwa kutangaza rasmi usajili huo mara tu baada ya mchezaji huyo kupitishwa katika vipimo vya afya na kukamilisha masuala ya kibali cha kazi.
Gyökeres anajiunga na kikosi chenye nyota kama Bukayo Saka, Martin Ødegaard, Gabriel Jesus na wengine, katika harakati za kutafuta taji la EPL ambalo wamekosa kwa zaidi ya miaka 20. Mashabiki wa Arsenal wamesubiri kwa hamu kuthibitishwa kwa usajili huo, ambao unaonekana kuwa wa kimkakati, hasa baada ya changamoto za msimu uliopita katika safu ya ushambuliaji.
0 Comments