Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima Media Dodoma
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imevitaka vyama vya siasa pamoja na wafuasi wao kuhakikisha kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 zinafanyika kwa amani, ustaarabu na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia na mshikamano wa kitaifa.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Jacobs Mwambegele, wakati akifungua Mkutano wa Kitaifa kati ya INEC na Vyama vya Siasa, ulioandaliwa kwa ajili ya kutoa taarifa za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 na kujadiliana na wadau juu ya miongozo na taratibu zitakazotumika.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi wa juu wa vyama mbalimbali vya siasa wakiwemo Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chaumma Hashim Rungwe, na Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Shaibu Addo, miongoni mwa wengine.
“Vyama vya siasa ninyi ndio mnaobeba dhamana ya moja kwa moja ya uchaguzi ushirikiano wenu ndio msingi wa uchaguzi wenye tija na unaoaminika kwa Watanzania,” amesema Jaji Mwambegele.
Pia amesema kuwa ratiba rasmi ya uchaguzi tayari imetolewa, ikiwa ni pamoja na tarehe za utoaji wa fomu za kugombea nafasi za urais, ubunge na udiwani, pamoja na muda wa kampeni Kwa wagombea waluopitishwa na vyama vyao
Ameeleza kuwa taratibu zote za kisheria zitazingatiwa ili kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mgombea.
“Tume imejipanga kuhakikisha kwamba kila chama na kila mgombea anapata haki sawa. Tutaendesha uchaguzi kwa uwazi, uhuru na haki kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Katika kuhimiza siasa safi, Jaji Mwambegele ametoa rai kwa vyama vyote kufanya kampeni kwa amani, kuepuka lugha za uchochezi na vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa taifa.
“Tume haivumilii aina yoyote ya uvunjifu wa amani. Tunatoa wito kwa wagombea na wanachama wa vyama vyote kuendesha kampeni za kistaarabu kwa heshima na uvumilivu.”
Amesema katika Kipindi cha kampeni kunakuwa na joto kali la kisiasa linalotokana na baadhi ya watu kukosa uvumilivu wa kisiasa hali ambayo inaweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.
"Napenda kutoa rai kwenu na wafuasi wenu kwa kuwasihi kufanya kampeni za kistaarabu na hivyo kuepuka kufanya vitendo vitakavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi yetu, " Amesema
Aidha ameyataja majimbo yatakayotumika kwenye uchaguzi ni 272 ambapo majimbo 222 yapo Tanzania Bara na Majimbo 50 yapo Tanzania Zanzibar
"Idadi hii ya majimbo ya uchaguzi kuna ongezeko la majimbo nane (08) yaliyoanzishwa kwa upande wa Tanzania Bara, " Amesema
Amesema, jumla ya Kata 3,960 zitafanya uchaguzi wa Madiwani, idadi hii kuna ongezeko la kata tano (05) zilizoongeka baada ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuanzisha kata mpya tano .
Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Addo Shaibu, ameipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa kuondoa Wakurugenzi wa Halmashauri na makada wa vyama katika usimamizi wa uchaguzi, akisema ni hatua ya kuongeza uaminifu wa mchakato huo.
Aidha, ameitaka Tume kuhakikisha vifaa vyote vya uchaguzi vinawafikia mawakala wa vyama kwa wakati, na kudhibiti upungufu wa nakala za nyaraka muhimu kama fomu za matokeo.
Addo pia ameeleza wasiwasi juu ya udhibiti hafifu wa karatasi za kupigia kura, na kuomba vyombo vya usalama, hasa Jeshi la Polisi, vihusishwe kikamilifu katika ulinzi wa vifaa vya uchaguzi.
“Uchaguzi huu ni wa kipekee. Tunashiriki kwa maslahi mapana ya taifa letu. Tuwe na uchaguzi huru, wa haki na unaoaminika,” amesema.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha UDP, Swaumu Rashidi, amepongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa kuonyesha usikivu kwa wananchi kwa kuongeza muda wa uandikishaji wa wapiga kura, hatua iliyochangia ongezeko kubwa la waliojiandikisha.
“Kuongezeka kwa wapiga kura si jambo la bahati mbaya, bali ni matokeo ya usikivu wa Tume na juhudi za kutoa elimu kwa wananchi. Utaratibu huu unapaswa kuendelezwa hadi kwenye hatua ya kuhamasisha wapiga kura wajitokeze siku ya kupiga kura,” amesema.
Swaumu pia ametoa rai kwa Tume kuheshimu maamuzi ya vyama pale makao makuu yanapowasilisha jina la mgombea, na kuepuka utenguzi wa wagombea kiholela.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kutenganisha majukumu ya Tume na vyama katika kutoa elimu kwa mawakala, ili kuepusha migongano isiyo ya lazima wakati wa uchaguzi.
0 Comments