Na. Mwandishi Wetu.
Kupatikana kwa sheria mpya na rafiki ya habari visiwani Zanzibar kutasaidia kuweka mazingira bora ya kazi kwa waandishi wa habari, kwa kuhakikisha ulinzi na ushiriki wao unapatikana kikamilifu hususan katika kipindi cha uchaguzi.
Akizungumza katika mkutano maalum ulioandaliwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na Kamati ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) huko Tunguu, Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ, Dkt. Mzuri Issa, amesema kuwa ni haki ya waandishi wa habari kuwekewa mazingira bora ya kazi.
Alisisitiza kuwa kuwepo kwa sheria rafiki ya habari kutawawezesha waandishi kufanya kazi kwa uhuru, ufanisi, na kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao.
Amesema kuwa kwa sasa teknolojia ya habari imekuwa kwa kasi, na idadi ya vyombo vya habari, hususan vya binafsi, imeongezeka kwa kiwango kikubwa.
Hata hivyo, licha ya maendeleo hayo, waandishi wa habari bado wanalazimika kufanya kazi kwa kutumia sheria zilizotungwa tangu mwaka 1988, ambazo hazina mlingano na mahitaji ya sasa ya taaluma ya uandishi wa habari pamoja na mazingira mapya ya kidijitali.
“Sheria zilitungwa kipindi hicho zilikuwa zinategemea siasa ya ujamaa na kujitegemea ambapo kwa sasa tasnia ya habari imekuwa kiteknolojia zaidi hivyo ushirikiano wa pamoja kwa mabadiliko unahitajika”, alisema Dkt Mzuri Issa.
Kwa upande wake Muwakilishi wa Jimbo la Pandani, Profesa Omar Fakih alieleza kuwa mabadiliko ya sheria za vyombo vya habari ni muhimu kwa maendeleo ya tasnia ya habari, hivyo ni vyema kuendelea kusimamia ili mswada uweze kufikishwa Barazani.
“Nilifanya jitihada binafsi kusaidia mswada kufikishwa Barazani lakini urasimu umechelewesha mchakato huo kukamilika”, aliongeza Profesa Omar.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Machano Othman, Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini, amesema kwamba wajibu wa Wawakilishi ni kujadili na kuibua masuala yanayogusa maisha ya wananchi.
Aidha, amebainisha kuwa waandishi wa habari wana haki ya kudai sheria mpya ya habari kwa kushirikiana kwa karibu na wadau wa sekta hiyo, ili kuhakikisha upatikanaji wa sheria iliyo rafiki na inayozingatia maslahi ya pande zote.
Kwa upande wao, Wajumbe wa ZAMECO wameeleza masikitiko yao kuhusu kucheleweshwa kwa kupatikana kwa sheria mpya ya habari Zanzibar, ambayo wamekuwa wakiidai kwa takriban miaka 20 sasa.
Wamesema kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha waandishi wa habari kushiriki katika chaguzi kuu bila kuwepo kwa sheria madhubuti itakayolinda haki na wajibu wao wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Mkutano huo umeandaliwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na Kamati ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO), kwa lengo la kuendeleza juhudi za utetezi na uchechemuzi wa kupatikana kwa sheria mpya na rafiki ya habari visiwani Zanzibar.
0 Comments