NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, ametoa siku 14 kwa wafanyabiashara zaidi ya 100 walioshinda zabuni ya vizimba na maeneo ya wazi katika Soko Kuu jipya la Mjini Kati kuanza rasmi shughuli za biashara, vinginevyo watachukuliwa hatua.
Agizo hilo limetolewa Julai 11, 2025, wakati wa ziara ya ukaguzi aliyoifanya katika soko hilo, ambapo alibaini kuwa maeneo 109 yaliyotolewa kwa njia ya zabuni kupitia mfumo wa kielektroniki wa TAUSI bado hayajaanza kutumika bila sababu za msingi.
“Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 26.6 katika ujenzi wa soko hili ili kuboresha mazingira ya biashara. Hatutakubali kuona maeneo haya yakikaliwa kimya wakati kuna wafanyabiashara wengi wanaohitaji nafasi,” alisema Mhe. Mtanda.
Katika ukaguzi huo, Mtanda pia alitoa wito kwa wafanyabiashara wanaoendesha shughuli katika maeneo yasiyo rasmi kuondoka mara moja na kurejea kwenye masoko yaliyopangwa, ili kulinda taswira ya jiji na kuhakikisha usafi na mpangilio wa mji.
“Hatuwezi kukaa kimya tukiruhusu uharibifu wa mazingira ya jiji. Wale wote wanaoziba barabara kwa kufanya biashara kiholela wachukuliwe hatua kali. Tunahitaji utaratibu ili kupanga vyema maendeleo yetu,” aliongeza.
Aidha Mtandao amefafanua kuhusu changamoto ya uhaba wa vizimba kwa baadhi ya wafanyabiashara, Mtanda alieleza kuwa kutokana na idadi kubwa ya wakazi wa jiji – zaidi ya milioni 1 kati ya milioni 3.6 wa Mkoa mzima – si rahisi maeneo 1,464 ya soko hilo kuwatosheleza wote kwa sasa. Hata hivyo, alibainisha kuwa kuna mipango ya ujenzi wa masoko mengine ili kukabiliana na ongezeko hilo.
Kwa upande wake, Afisa Biashara wa Jiji la Mwanza, Madelina Mtweve, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Jiji, alisema kuwa mnamo mwaka 2018/19 wafanyabiashara 807 walihamishwa kutoka soko la zamani kupisha ujenzi wa soko la kisasa ulioanza rasmi mwaka 2019/20.
Bi. Mtweve alifafanua kuwa soko jipya lina jumla ya maduka 522, vizimba, meza 504, mabucha, migahawa midogo 12, machinjio 167, stoo 15, vyoo vitatu vyenye matundu ya kutosha pamoja na eneo la maegesho ya magari 159.
0 Comments