Header Ads Widget

ROSTAM AZIZI ATOA WITO WA UWEKEZAJI KATIKA VYOMBO VYA HABARI VYA KISASA

 


Na Pamela Mollel, Arusha

Katika kongamano la pili la Mabaraza ya Habari Barani Afrika lililofanyika jijini Arusha, mfanyabiashara maarufu Rostam Azizi ametoa wito kwa serikali, sekta binafsi na wadau wa habari kuwekeza katika vyombo vya habari vya kidijitali vinavyotumia teknolojia ya kisasa kama akili bandia (AI).

Hotuba hiyo ilisomwa kwa niaba yake na Absalom Kibanda, ambapo Rostam alieleza safari ya zaidi ya miaka 30 ya vyombo binafsi vya habari nchini Tanzania tangu kuanzishwa kwake miaka ya 1990.

Aliwatambua waanzilishi wa vyombo hivyo akiwemo Reginald Mengi na Jenerali Ulimwengu, huku akieleza mchango wake binafsi katika kuanzisha Mwananchi Communications na baadaye New Habari (2006) Ltd.

Rostam alisisitiza kuwa vyombo vya habari vimekuwa nguzo muhimu ya taifa, hasa katika zama hizi za mitandao ya kijamii na taarifa za mtandaoni, ambako vita vya taarifa vinachezwa kwa kutumia “algorithms” badala ya silaha.


“Leo, kila simu ni kipaza sauti, na kila 'like' ni kura ya maoni,” alieleza Kibanda kwa niaba yake, akiitaka Tanzania kuwekeza katika majukwaa ya kisasa yatakayowezesha simulizi za kizalendo kwa lugha ya ubunifu na maadili.

Aliongeza kuwa vyombo vya habari ni sehemu ya miundombinu muhimu ya taifa kama ilivyo kwa viwanda na barabara, kwani ndivyo vinavyofinyanga fikra na taswira ya taifa kimataifa.

Alitamatisha kwa kusema kuwa “hili si suala tu la usalama wa taifa, bali ni suala la uhuru wa kifikra na wa kitaifa.”

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI