Header Ads Widget

DCEA NA TANAPA WATEKETEZA MASHAMBA YA BANGI EKARI 614 KATIKA USHOROBA WA MIKUMI-NYERERE.

Na Matukio Daima Media

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na TANAPA na wananchi wa maeneo ya jirani, kuanzia tarehe 6 hadi 15 Julai, 2025 wamefanya operesheni mkoani Morogoro, hususan kwenye ushoroba kati ya Hifadhi za Taifa za Mikumi na Nyerere. Katika operesheni hiyo, ekari 614 za mashamba ya bangi ziliteketezwa, kilogramu 3,741.9 za bangi kavu na kilogramu 1,706 za mbegu za bangi zilikamatwa na kambi 72 za wakulima wa bangi zilisambaratishwa huku watuhumiwa tisa (9) wakikamatwa.

Akizungumza katika eneo la operesheni, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo, alisema kuwa operesheni hiyo ni sehemu ya mapambano endelevu dhidi ya dawa za kulevya nchini, hususan katika maeneo yanayozunguka hifadhi za taifa ambapo baadhi ya wahalifu wamekuwa wakijificha na kulima bangi.

“Operesheni hii imeonesha mafanikio makubwa. Mashamba ya bangi yamepungua ikilinganishwa na awali na wakulima wa bangi wameendelea kusogea mbali zaidi na hivyo kuonesha kwamba operesheni tunazofanya zinaleta mafanikio chanya” alisema Kamishna Jenerali Lyimo.

Aidha, amesema kwamba, Mamlaka itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali na vyombo vya ulinzi na usalama kudhibiti maeneo yote yanayotumika kwa kilimo haramu cha bangi na kutoa elimu kwa wananchi wa maeneo hayo ili kujenga uelewa juu ya madhara ya dawa za kulevya hususan bangi, pamoja na kuwahamasisha kutafuta shughuli mbadala zitakazowaingizia kipato halali.

“Hatuwezi kuruhusu dawa za kulevya ziendelea kuharibu jamii yetu. Tunawaomba wananchi wote waendelee kushirikiana nasi kwa kutoa taarifa ili kuhakikisha tunamaliza kabisa tatizo hili,” alisisitiza Kamishna Lyimo.

Kwa upande wake, Moses Oko Onyango, Kamanda Mkuu Msaidizi Kikosi TANAPA akimwakilisha Mkuu wa Hifadhi ya Nyerere, alisema kuwa, baada ya kupata taarifa kuhusu kuwepo kwa mashamba makubwa la bangi katika eneo la Nyarutanga, karibu na mipaka ya Hifadhi za Nyerere na Mikumi, waliona ni vema kushiriki kwenye zoezi hilo kwani DCEA na TANAPA ni taasisi za serikali ambazo zinapaswa kushirikiana kila mara kunapokuwa na changamoto za aina hiyo.

“TANAPA inalinda uhifadhi endelevu wa maliasili, hatutakubali watu kutumia maeneo ya hifadhi kwa shughuli haramu. Kwa kushirikiana na Mamlaka tutaongeza nguvu ya kudhibiti uhalifu kwenye ushoroba” alisema Onyango.

Aliongeza kuwa, kupitia Kitengo cha Mahusiano na Jamii, TANAPA iko tayari kushirikiana na DCEA katika kutoa elimu kwa jamii, mashuleni na vijijini kuhusu athari za bangi na umuhimu wa kulinda mazingira. Aidha, TANAPA itashirikiana na Mamlaka kufanya doria za pamoja katika maeneo yanayozunguka hifadhi ili kudhibiti kilimo haramu cha bangi.

Mamlaka inaendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa ili kuhakikisha kuwa kilimo na biashara ya dawa za kulevya inakomeshwa kabisa na jamii inalindwa dhidi ya madhara ya dawa hizo.

End. 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI