Header Ads Widget

RC KIHONGOSI AZINDUA MSIMU WA PILI WA ARUSHA JOGGING SPORTS CLUB AHIMIZA AMANI NA MSHIKAMANO

Na Pamela Mollel,Arusha 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Kenan Kihongosi, leo Julai 19, 2025, ameongoza mamia ya wakazi wa Arusha kushiriki mazoezi ya pamoja ya kukimbia kupitia programu ya Arusha Jogging Sports Clubz ambapo pia alizindua rasmi msimu wa pili wa mazoezi hayo ya kijamii 

Mazoezi hayo ya kilomita 10 yaliandaliwa na Arusha Jogging Club, yakihusisha wakazi wa jiji la Arusha, viongozi mbalimbali wa serikali, na wanachama wa klabu hiyo. 

Mbio zilianzia ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kupita Clock Tower, kuelekea Mianzini, na kurudi tena ofisini kwa Mkuu wa Mkoa, zikiongozwa na kikosi cha usalama barabarani.

Akizungumza baada ya mazoezi, Mhe. Kihongosi alisisitiza umuhimu wa kudumisha mshikamano, amani na upendo miongoni mwa wakazi wa jiji la Arusha, bila kujali tofauti za kidini, kikabila au kiitikadi. 

Alitoa wito kwa wananchi kuwaepuka watu wanaotaka kueneza chuki na kuwagawa wananchi kwa maslahi binafsi.



“Huna sababu ya kumchukia yeyote wala kumuumiza kwa sababu kesho yako huijui. Kila mtu hapa ana familia, matatizo, na watu wanaomtegemea. Kuwa baraka katika maisha ya watu,” alisema.


Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu mwezi Oktoba, Mkuu huyo wa Mkoa aliwasihi wakazi wa Arusha kujitokeza kwa wingi kupiga kura, huku akipinga vikali ushawishi wa watu wanaotaka kuwavunja moyo wasishiriki katika uchaguzi huo.

“Usipande miba kwenye njia ya mtu, kwa sababu siku moja utapita peku nayo itakuchoma,” aliongeza kwa mafumbo yenye ujumbe mzito wa kijamii.



Uzinduzi wa msimu huu wa pili wa Arusha Jogging Sports club umepokelewa kwa shangwe kubwa na wakazi wa Arusha, ambapo wengi wameelezea kuwa mazoezi hayo si tu yanachangia afya bora, bali pia ni jukwaa la kukuza mshikamano, uzalendo na maadili ya kijamii. 



Mkuu wa Mkoa pia alitoa pongezi kwa uongozi wa Arusha Jogging Club kwa juhudi zao katika kuhamasisha mazoezi na afya ya jamii kwa njia chanya na ya kijumuishi.


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI