Maafisa na Askari 70 wa Jeshi la Uhifadhi la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutoka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, wamevishwa vyeo vipya na kutakiwa kuongeza ubunifu, weledi na kutumia teknolojia ya kisasa katika kulinda rasilimali za misitu nchini.
Zoezi la kuwapandisha vyeo maofisa hao limefanyika leo Julai 19, 2025 katika Ofisi za Shamba la Miti Sao Hill mkoani Iringa, likiongozwa na Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa Kanda hiyo, Getrude Nganyagwa, aliyemwakilisha Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Nganyagwa alisema kupandishwa cheo ni dhamana kubwa inayopaswa kwenda sambamba na ufanisi, uadilifu na kuonyesha mfano bora kwa askari wengine.
“Kupanda cheo siyo tu heshima, bali ni wito wa kuwa kiongozi mwenye maono, nidhamu na uwezo wa kuongoza wenzako katika kutekeleza majukumu ya kitaasisi,” alisema.
Alisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia ya kisasa katika utendaji kazi, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya ufuatiliaji wa matukio ya moto, doria za kijeshi na uhifadhi wa takwimu muhimu za misitu.
Katika kuelekea msimu wa kiangazi unaosababisha matukio mengi ya moto, Nganyagwa aliwataka maafisa hao kushirikiana na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi ili kuimarisha ulinzi wa misitu na kuhakikisha usalama wa mazingira.
“Hali ya hewa ya sasa inahitaji tahadhari kubwa. Ushirikiano kati yenu na wananchi walioko jirani na hifadhi ni jambo la msingi ili kuzuia uharibifu wa misitu unaoweza kusababisha madhara makubwa ya kiikolojia na kijamii,” alisema.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoramu, aliwapongeza askari na maafisa waliovishwa vyeo, akisisitiza kuwa hatua hiyo isiishie kuwa heshima ya binafsi bali iwe chachu ya kuongeza bidii na ufanisi kazini.
“Kupanda cheo si bahati nasibu; ni matokeo ya utendaji mzuri. Tunapaswa kuongeza nguvu kazini huku tukizingatia weledi, nidhamu na mshikamano,” alisema PCO Yoramu.
Askari waliovishwa vyeo wanatoka katika vituo vya uhifadhi vya Njombe, Makete, Ludewa, Wanging’ombe, Mufindi, Kilolo, pamoja na Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Uzungwa, Kilombero, na Shamba la Miti Sao Hill.
0 Comments