Header Ads Widget

RC KIHONGOSI ATAJA MAFANIKIO MAKUBWA ARUSHA ASISITIZA UREJESHAJI MIKOPO YA HALMASHAURI

Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima Media – Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi, amevitaka vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilivyopewa mikopo kupitia halmashauri za mkoa huo kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuwezesha vikundi vingine kupata fursa sawa.


Akizungumza jijini Dodoma leo Julai 20, 2025, wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Kihongosi alisema hali ya urejeshaji wa mikopo imekuwa changamoto kubwa kwa baadhi ya wanufaika.

Alisema fedha zinazotolewa ni sehemu ya kodi za wananchi, hivyo ni wajibu wa kila mnufaika kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa ili zitumike tena kwa walengwa wengine walioko kwenye orodha ya kusubiri.

Aidha amesema Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, idadi ya vikundi vilivyonufaika na mikopo hiyo imeongezeka kutoka vikundi 721 mwaka 2021 hadi kufikia vikundi 1,380 mwaka 2025 na mikopo hiyo hutolewa bila riba kwa mujibu wa mwongozo wa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.

"Baadhi ya vikundi vilivyofaidika ni pamoja na kikundi cha vijana cha USA River, ambacho kilipokea mkopo wa shilingi milioni 100 kutoka Halmashauri ya Meru na kuweza kununua gari aina ya Coaster kwa ajili ya biashara ya usafirishaji, " Amesema

"Kikundi cha wanawake wafugaji kutoka Halmashauri ya Arusha kilipokea shilingi milioni 35 na kuanzisha kiwanda kidogo cha kutengeneza mikate (bakery), " Amesema 

Kihongosi ameeleza kuwa hadi kufikia mwaka 2025, kiasi cha mikopo iliyotolewa kimeongezeka kutoka shilingi bilioni 3.08 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi bilioni 13.55, ikiwa ni zaidi ya mara nne ya kiwango cha awali.

Katika hatua nyingine, Mkoa wa Arusha umepokea zaidi ya shilingi bilioni 57.22 kutoka Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 38.39 zilitumika kwa ajili ya kuwahudumia moja kwa moja walengwa wa mpango huo kupitia uhawilishaji wa fedha, na shilingi bilioni 18.82 zilitumika kwenye utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya jamii.

Aidha, mapato ya ndani ya halmashauri yameongezeka kwa kasi kutoka shilingi bilioni 34.63 mwaka 2020/21 hadi shilingi bilioni 110.12 mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 318, hali inayochochea uwezo wa halmashauri katika kujiendesha na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kujitegemea.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mapato ya ndani umeongezeka kutoka shilingi bilioni 16.37 mwaka 2020/21 hadi bilioni 40.48 mwaka 2024/25, hatua inayochochea ustawi wa kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI