Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene amewaonya wale wote wanaohamasisha uvunjifu wa amani nchini huku akiwasihi Wanawake wasijiingize kwenye mtego huo kwani madhara yake ni makubwa.
Mhe.Simbachawene ametoa kauli hiyo leo wakati akifungua Kongamano la 16 la Wanawake Waombolezao Kitaifa waliokusanyika jijini Dodoma kwa ajili ya kuombea amani ya nchi ya Tanzania hususan katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Amesema maendeleo yaliyopo nchini ikiwemo huduma za kijamii ni matokeo ya amani na utulivu uliopo, "Hatuwezi kubomoa ili tujenge upya, ni lazima tukumbatie majadiliano kama Taifa hatuwezi tukawa tunafikiria sawa ni lazima tutofautiane" amesisitiza Mhe. Simbachawene.
"Kuna watu wanasema Tanzania hii hakuna amani wala maendeleo yaliyofanyika tangu tupate uhuru, hivyo tuandamane, hapo ndipo tutapata haki yetu, wananchi kataeni huo ushetani" amesema Waziri Simbachawene
Kufuatia hatua hiyo Mhe.Simbachawene amewataka Watanzania kuwapuuza wale wote wenye maslahi binafsi wanaotaka kuwaona wananchi wanachukiana wenyewe kwa wenyewe na hatimaye kuanza kuuana wao kwa wao kwa chuki za kupandikizwa.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Tanzania Fellowship of Churches, Godfrey Malasi amesema Kongamano hilo ni mahsusi kwa ajili ya maombi maalum ambayo yamekuwa yakifanyika kila mwisho wa mwaka kwa lengo la kuliombea amani Taifa la Tanzania na kuwahimiza Watanzania kumjua na kumtumikia Mungu.
Sisi tunavyofurahia amani na utulivu tuliyonayo, wenzetu huko kwingine wanalia na kusaga meno, hivyo tuna wajibu wa kuzidi kumuomba Mungu atupe hekima ili tuzidi kuilinda amani yetu, amesisitiza Askofu Malasi.
Vita sio nzuri kabisa, sisi tumepewa uwezo wa kupigana vita vya rohoni ili kuzuia vita vinavyoonekana " amesema
Aidha, Askofu Malasi amesema Kongamano hilo limekuwa likiombea maadili mema ya Taifa hususan katika kipindi hiki ambacho vijana wameathiriwa na vitendo vya ushoga, usagaji na utoaji mimba, vitendo ambavyo vinakwenda kinyume na tamaduni zetu.
0 Comments