Haya ni wimbi kubwa la maandamano ambayo nchi hiyo imeshuhudia katika miaka ya hivi karibuni.
Takriban watu 22, akiwemo afisa wa polisi, wameuawa na wengine 200 kujeruhiwa katika maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya mafuta yaliyoanza Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Ndani Manuel Homem amesema.
Polisi wanasema zaidi ya watu 1,200 pia wametiwa mbaroni katika kile kilichoanza kama mgomo wa madereva wa teksi kupinga kupandishwa kwa bei na kisha kushika kasi na kuwa moja ya wimbi kubwa la maandamano ambayo nchi hiyo imewahi kuyashuhudia katika miaka ya hivi karibuni.
Biashara, pamoja na maduka makubwa, zimesalia kufungwa na watu wengi wamechagua kukaa nyumbani.
Madaktari katika hospitali za umma katika mji mkuu, Luanda ambao hawakutaka kutajwa majina waliiambia BBC kuwa huduma za dharura zimezidiwa katika muda wa saa 24 zilizopita.
Siku ya Jumatatu na Jumanne milio ya risasi ya hapa na pale ilisikika katika jiji lote.
"Tumepokea waandamanaji wengi wakiwa na majeraha mabaya, ikiwa ni pamoja na majeraha mengi. Cha kusikitisha ni kwamba wengine wamefariki. Tunahofia huenda idadi ya waliofariki ikawa kubwa kuliko takwimu rasmi zinavyopendekeza," daktari mmoja alisema.
0 Comments