Header Ads Widget

KOMBE LA DUNIA VILABU: JE, MWAROBAINI WA PSG UMEPATIKANA?

 

Chelsea sasa wameshinda Kombe la Dunia la Vilabu mara mbili, mara yao ya awali ni 2021

Paris St-Germain imekuwa ikikusanya mataji ya msimu, kuanzia taji la Ligue 1 mapema Aprili hadi kuibomoa Inter Milan katika fainali ya Ligi ya Mabingwa. Pia wameifunga Bayern Munich wakiwa na watu tisa na kisha kuwalaza Real Madrid 4-0 katika nusu fainali ya kombe la dunia la vilabu.

Na walipigiwa upatu kuifunga Chelsea huko New Jersey, Marekani, lakini wakati huu ni WaParisi ndio waliobaki wamepigwa na butwaa.

Hata kabla ya kipindi cha mapumziko, Cole Palmer alifunga mabao mawili na kutengeneza jingine kwa Joao Pedro na kuwaweka The Blues mbele kwa mabao 3-0. Na ndivyo mechi ilivyoisha.

Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca aliwezaje? Na Chelsea wako vizuri kiasi gani?

Kama ilivyo katika miaka miwili iliyopita, kucheza vizuri kwa Palmer kunamaanisha Chelsea inacheza vizuri.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 amekuwa akicheza chini ya kiwango katika mechi akiwa namba 10 katika msimu huu. Wakati fulani alicheza mechi 18 bila kufunga bao na hivi karibuni alikiri kuwa alipitia "wakati mgumu ndani na nje ya uwanja".

Hata hivyo, baada ya kurejeshwa upande wa kulia wakati wa mchuano huu - nafasi aliyoizoea chini ya bosi wa awali Mauricio Pochettino – ameonekana kurudi katika ubora wake tena.

"Mbinu yetu ilikuwa ni kucheza mtu na mtu kwa sababu ukiacha nafasi kwa PSG watakuua, kwa hivyo tulijaribu kucheza kwa nguvu na kuwakosesha nafasi na mbinu hiyo ilikuwa muhimu katika dakika 10 za kwanza," anasema Maresca.

Mara baada ya Chelsea kuzibiti mchezo, ilikuwa wazi kwamba wana nia ya kutumia upande wa kushoto wa PSG, kwani Joao Pedro mara kwa mara alikuwa akienda kuungana na Palmer.

Mbinu yao mara nyingi ilikuwa ya moja kwa moja, pasi zikipigwa mbele ya walinzi wa PSG, lakini beki wa kushoto Nuno Mendes ndiye aliyekuwa na wakati mgumu zaidi.

"Tulipata mafanikio mengi kwa kutumia upande wa kushoto wa safu yao ya ulinzi," amesema Maresca. "Mambo yalikwenda vizuri kutokana na juhudi za wachezaji."

Kombe la Dunia la Vilabu

Kumekuwa na mijadala mingi kuhusu jinsi shindano hili jipya lilivyopanuliwa. Lakini Chelsea watabaki kujiita mabingwa hadi shindano lijalo lichezwe, lililopangwa kufanyika 2029. Na lina thamani ya kati ya pauni milioni 80 na £90m kama za zawadi.

"Ninahisi shindano hili litakuwa muhimu kama au muhimu zaidi kuliko Ligi ya Mabingwa," amesema Maresca.

"Nilikuwa na bahati ya kuwa sehemu ya wakufunzi [Manchester City] ambao walishinda Ligi ya Mabingwa miaka mitatu iliyopita, lakini shindano hili linashirikisha vilabu bora zaidi duniani. Ndiyo maana tunalithamini sana kama vile Ligi ya Mabingwa, au pengine hata zaidi.

"Kwetu sisi, ulikuwa ushindi mkubwa. Kuwaruhusu mashabiki wa Chelsea kuvaa ubingwa wa dunia kwenye jezi zao, ni chanzo cha fahari kwetu."

Timu ya Chelsea


Mmiliki mwenza wa Chelsea, Todd Boehly akipeana mikono na meneja Enzo Maresca kwenye jukwaa baada ya mchezo kumalizika

Wengi wamecheka juu ya usajili kwa Chelsea chini ya Todd Boehly. Wametumia kiasi cha pauni bilioni 1.5 kununua wachezaji tangu aichukue mwaka 2022 - na wachezaji wamepewa mikataba ya miaka mingi, kama miaka saba, minane na tisa.

Miezi 18 iliyopita walipoteza katika fainali ya Kombe la Carabao kwa Liverpool. Lakini katika Kombe la Dunia la Klabu mwaka huu wanaonekana wako vizuri.

Walikuwa na kikosi cha vijana zaidi ya timu yoyote kwenye Kombe la Dunia la Vilabu, bila mchezaji mwenye umri wa zaidi ya miaka 27. Hivyo hilo linawafanya kuwa bora zaidi.

Ripota wa BBC Sport Nizaar Kinsella, ambaye alikuwa akitazama mechi kwenye Uwanja wa MetLife, amesema: "Chelsea ina utulivu kwa mara ya kwanza tangu serikali ya Uingereza kumuwekea vikwazo Roman Abramovich baada ya vita vya Ukraine kuanza Machi 2022.”

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI