Na chausiku said
Matukio Daima Media Mwanza.
ampuni ya uzalishaji wa filamu Kingdom Fighter imefanya usaili kwa ajili ya kupata waigizaji wapya watakaoigiza katika tamthilia mpya itakayoanza hivi karibuni Mkoani Mwanza, ikiwa ni juhudi za kuinua vipaji vya wasanii wa filamu na kuleta mapinduzi ya tasnia hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza jana wakati wa zoezi la usaili, Mkurugenzi wa Kingdom Fighter, Edward Emmanuel, alisema lengo ni kuwainua wasanii wa filamu wa Mwanza na kuwarudisha katika ramani ya burudani nchini.
"Lengo letu ni kuinua vipaji vya wasanii wetu wa Mwanza na kuendeleza yale mazuri ambayo waigizaji wetu wa zamani walikuwa nayo. Mwanza ina vipaji, lakini changamoto kubwa ni kazi nyingi kutofikia ubora wa kuonekana kwenye televisheni kubwa,” alisema Emmanuel.
Emmanuel ameeleza kuwa tamthilia mpya inayotarajiwa kuanza kurekodiwa hivi karibuni itajumuisha waigizaji wengi kutoka Mwanza, wakiwemo maarufu, pamoja na kushirikiana na wakongwe kutoka Dar es Salaam.
Aidha amefafanu kuwa moja ya sababu ya kazi nyingi za Kanda ya Ziwa kushindwa kufika mbali ni ukosefu wa maandalizi ya kitaalamu, ikiwemo uandishi wa script, maandalizi ya makubaliano rasmi, na kushindwa kuelewa mahitaji ya vituo vya runinga.
“Tofauti na wengine, sisi tumepitia hatua zote za maandalizi, tumehakikisha tuna script zilizoandikwa na waandishi wakubwa, tumejadiliana na vituo vya televisheni na tuko tayari kuanza kurekodi kwa ubora unaotakiwa,” aliongeza.
Emmanuel pia alieleza kuwa changamoto nyingine ni baadhi ya wasanii kutotekeleza makubaliano ya kurekodi vipande vya tamthilia (scene), hali inayosababisha kazi kutokamilika kwa wakati.
“Tumejipanga kisheria kuhakikisha msanii anapokubaliana kushiriki, anazingatia makubaliano. Tunahitaji kuwa na mikataba ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza baada ya kazi kwenda hewani,” alisema.
Kwa upande mwingine, alisema serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan imetoa mazingira rafiki kwa sekta ya sanaa kwa kutoa mikopo kwa wazalishaji wa maudhui, hivyo wasanii wanapaswa kuelewa kuwa filamu ni ajira rasmi na chanzo halali cha kipato.
Naye Meneja wa programu ya tamthilia hiyo mpya, Daddy Mawala, alisema usaili unafanyika kwa kuzingatia uwezo na vipaji halisi, na siyo kwa misingi ya sura au mahusiano ya karibu.
“Tumekuwa tukipoteza ubora kwa sababu ya kuingiza watu kwa kufahamiana. Sasa tunahitaji ubora unaotokana na uwezo wa kweli wa kuigiza. Lengo letu ni kuinua vipaji vya hapa Mwanza kwa kiwango cha kitaifa,” alisema Mawala.
Baadhi ya waigizaji waliojitokeza kushiriki usaili wa kupata nafasi katika tamthilia mpya inayotarajiwa kuanza, wameeleza kuwa ujio wa tamthilia hiyo ni fursa adhimu ya kuwaendeleza kiuchumi na kukuza vipaji vyao vya sanaa.
Wasanii hao wamepongeza juhudi zinazofanywa na kampuni ya Kingdom Fighter na kueleza kuwa tamthilia hiyo inakuja wakati mwafaka ambapo fursa za kazi kwa wasanii wa hapa jijini zimekuwa finyu kwa muda mrefu.
“Tunaamini ujio wa tamthilia hii utatufungulia milango ya mafanikio, tumehangaika kwa muda mrefu bila mafanikio, lakini sasa tunaiona nuru,” walieleza.
Hata hivyo, wasanii hao wameeleza changamoto kadhaa zinazokwamisha maendeleo ya sanaa jijini Mwanza, ikiwemo uongozi duni wa baadhi ya waongozaji wa filamu, kutokuwepo kwa mshikamano miongoni mwao, na tabia ya baadhi ya wasanii kutokuwa waaminifu au kushindwa kujitokeza kwenye kazi za pamoja.
“Sanaa yetu hapa Mwanza ikilinganishwa na maeneo mengine, utaona kabisa sisi tunajitolea na tunafanya kazi kwa bidii, lakini bado hatufikii mbali kwa sababu hatuna umoja wa kweli na hatujitokezi kikamilifu kwenye kazi,” Walieleza.
Meneja huyo aliwataka wasanii wote kujitokeza kwa wingi katika usaili huo, huku akisisitiza kuwa kila msanii atapewa haki yake na hakuna atakayesikitika endapo atachaguliwa au hata kama hatapata nafasi.
0 Comments