Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WANANCHI wa mkoa Kigoma wamesema kuwa kambi za huduma za matibabu ya Kibingwa zinazofanyika kwenye maeneo mbalimbali mkoani humo yamekuwa msaada mkubwa kwa kuwezesha kusogezwa karibu kwa huduma hizo sambamba na kupunguza gharama kwa wananchi wanaohudhuria kupata matibabu kwenye kambi hizo.
Hayo yameelezwa wakati wa kufungwa kwa kambi ya matibabu iliyokuwa ikisimamiwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Empower Society, Building the Nation (ESBN) yaliyofanyika katika mji mdogo wa Uvinza mkoani Kigoma ambapo huduma hizo zilikuwa zikitolewa bila malipo.
Mmoja wa wananchi hao Robinson Bakayemba mkazi wa Uvinza mkoani Kigoma ambaye alihudhuria huduma za matibabu katika kambi hiyo alisema kuwa imewarahisishia na kuwasogozea huduma karibu lakini pia katika kambi hiyo hawakulipa gharama zozote za vipimo, ushauri wala dawa waliozokuwa wakipewa.
Naye Zuhura Chubwa mkazi wa kitongoji cha Kashakari mji mdogo wa Uvinza mkoani Kigoma alisema kuwa kwa muda mrefu alikuwa anasumbuliwa na tumbo lakini hakuwa na fedha na hospitali ya wilaya Uvinza kuna umbali Zaidi ya kilometa 20 hivyo ujio wa madaktari hao umewezesha kufanyiwa uchunguzi na kupata matibabu.
Akieleza kuhusu uwepo wa kambi hiyo ya madaktari Bingwa inayotembea Mratibu wa huduma hizo, Mbwana Mwinyi Mkuu ambaye ni Afisa utafiti kutoka taasisi ya ESBN alisema kuwa kambi hiyo ya Uvinza mkoani Kigoma ni ya pili kwa mwaka huu baada ya ile ya awali iliyofanyika wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.
0 Comments