Header Ads Widget

CCM KUFANYA MAREKEBISHO MADOGO YA KATIBA KUPITIA MKUTANO WA MTANDAONI


 Na Hamida Ramadhan,Matukio DAIMA Media Dodoma

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kufanyika kwa Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho kesho kwa njia ya mtandao, kwa lengo la kujadili ajenda moja  ambayo ni marekebisho madogo ya Katiba ya chama.

Akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla,alisema mkutano huo umeitishwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Ibara ya 99(1)(a-f) na (2), ambayo inaruhusu kufanyika kwa mkutano wa aina hiyo pale panapokuwa na ulazima wa kufanya marekebisho ya katiba.

“Wanaoruhusiwa kufanya marekebisho ya Katiba ya CCM ni Mkutano Mkuu pekee. Na kwa kuwa uongozi umeona ipo haja ya kufanya marekebisho haya madogo, tumewaitisha Mkutano Maalum kwa njia ya mtandao,” alisema Makalla.

Akizungumzia namna mkutano huo utakavyofanyika, Makala alieleza kuwa maandalizi yamekamilika na teknolojia itatumika kwa ufanisi kuhakikisha wanachama wote wanaohusika wanashiriki bila changamoto.

“Kumekuwa na maswali mitandaoni kuhusu kwa nini tunafanya mkutano kwa njia ya mtandao. Ukweli ni kwamba dunia inabadilika na lazima twende sambamba na teknolojia Tunawahakikishia kuwa kila kitu kiko tayari na mkutano utaenda vizuri,” alisema.


Hata hivyo, Makala hakufafanua kwa undani ni vipengele gani vya Katiba vitafanyiwa marekebisho, lakini alisisitiza kuwa ni mabadiliko madogo yatakayowasilishwa kwa wanachama wa mkutano huo kwa ajili ya kupitishwa.

Mkutano huo wa aina yake unakuja katika kipindi ambacho vyama vya siasa nchini vinazidi kuimarisha miundombinu yao kwa kutumia teknolojia, ikiwa ni sehemu ya mageuzi ya kiuongozi na usimamizi wa shughuli za kisiasa nchini.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI