Na Hamida Ramadhan Matukio Daima App Kondoa
SHIRIKA la Foundation for Disabilities Hope (FDH) kwa ufadhili na Abilis Foundation, limeendesha mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake wenye ulemavu katika Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma, kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi na kuwaondoa katika utegemezi.
Mafunzo hayo ya siku mbili yalilenga kuwajengea washiriki ujuzi wa kutengeneza bidhaa mbalimbali kama sabuni, batiki, pamoja na mbinu za kuongeza thamani ya bidhaa hizo ili kuwa na ushindani sokoni.
Akizungumza mara baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa FDH, Maiko Salali, alisema kuwa wanawake 50 kutoka Wilaya ya Kondoa walinufaika na mafunzo hayo ya awali, huku lengo likiwa ni kuwafikia wanawake zaidi ya 300 katika wilaya hiyo.
“Tunashukuru Abilis Foundation kwa kufadhili mradi huu unaolenga kuwainua wanawake wenye ulemavu kutoka kwenye utegemezi hadi kuwa wajasiriamali wanaojitegemea. FDH tutaendelea kuwa bega kwa bega na jamii hii ili kuhakikisha wanajikwamua kiuchumi,” alisema Salali.
Kwa upande wake, Maurasa Shoo, mkufunzi kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) mkoa wa Dodoma, alisema mafunzo hayo yaliwahusisha watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali, ambapo asilimia 99 ya walengwa walihudhuria kikamilifu.
Shoo alisisitiza kuwa kila mtu ana nafasi ya kufanikiwa, bila kujali hali yake ya kimwili:
“Mafanikio hayana maumbile. Vyovyote ulivyo, unaweza kufanikisha ndoto zako. Serikali kupitia Halmashauri ina fursa nyingi za mitaji na mikopo, hivyo ni wakati wa kuchangamkia hizi nafasi,” alieleza Shoo.
Aidha, uongozi wa Wilaya ya Kondoa ulihudhuria mafunzo hayo, jambo linalotarajiwa kurahisisha upatikanaji wa mikopo ya asilimia 10 ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia Halmashauri.
Aidha, Mwenyekiti wa Shivyawata Wilaya ya Kondoa, Abeid Omary Duttu, aliipongeza FDH kwa kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika miradi ya maendeleo, akisema hatua hiyo imeanza kuvunja ukuta wa unyanyapaa na kuwaonesha walemavu kama watu wenye uwezo na haki sawa katika jamii.
“Kwa muda mrefu watu wenye ulemavu wamekuwa wakisahaulika kwenye mipango ya maendeleo. Lakini kupitia mradi huu, tunaanza kuonekana na kuthibitisha kuwa tunaweza kuchangia uchumi wa nchi kama wengine,” alisema Duttu.
Naye Julieth Anator Mtadilwa, ambaye ni mmoja wa wajumbe walioshiriki mafunzo hayo, alisema ameongeza maarifa ambayo yatamsaidia kuanzisha shughuli yake ya kiuchumi.
“Mafunzo haya yamenifungua macho. Najua sasa kutengeneza sabuni na kuongeza thamani ya bidhaa. Natoka hapa nikiwa na dira ya kujitegemea na kuwasaidia wengine,” alisema Julieth kwa furaha.
0 Comments