NA MATUKIO DAIMA APP.
DODOMA.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Julai 17, 2025 anatarajiwa kuzindua rasmi Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Mjini Dodoma, Akiwa Rais wa Pili kufanya hivyo mara baada ya Hayati Benjamin William Mkapa kuzindua Dira ya Taifa ya 2025 mnamo mwaka 2000.
Kulingana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo, Dira 2050 imeweka rekodi pia ya kuwa Dira yenye kuzingatia maoni mengi zaidi ya wananchi ambapo takribani wananchi Milioni 1.17 walifikiwa mmoja mmoja, wengine zaidi ya 20,000 walifikiwa kupitia makongamano na mikutano ya wadau mbalimbali sambamba na waliotoa maoni yao kupitia tovuti maalumu ya Tume ya Taifa ya Mipango.
Kuzinduliwa kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kulingana na Tume ya Taifa ya Mipango kunafuatia hatua muhimu ya Baraza la Mawaziri la serikali ya awamu ya sita kuidhinisha dira hiyo pamoja na kuridhiwa kwake kwa mara ya kwanza katika Historia na Bunge la Tanzania kama sehemu ya kutoa Kinga katika kutekelezwa kwake na kutokuachwa kando na serikali zitakaoongoza Tanzania kwa miaka 25 ljayo.
"Kwa mara ya pili nchi yetu inazindua Dira ya maendeleo ya Taifa ambayo haina mwelekeo wa kiitikadi ya Chama cha siasa na Rais Samia Suluhu Hassan anakuwa Rais wa Pili kuandika Dira ya Taifa, Rais wa kwanza alikuwa Hayati Rais Benjamini William Mkapa." Amesema Prof. Kitila.
Pamoja na mambo mengine, malengo ya Dira mpya ya Taifa ya mwaka 2050 kulingana na serikali ni kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi jumuishi unaopunguza umasikini, unaozalisha ajira na kuchochea mauzo ya nje ya bidhaa, kuongeza tija katika uzalishaji sambamba na uongezaji wa thamani kwenye mifugo, madini, misitu pamoja na kilimo.
Aidha takwimu za maoni ya wananchi yaliyokusanywa kuhusu Dira Taifa ya Maendeleo 2050 zinaonesha kuwa idadi kubwa ya wananchi waliofikiwa na timu ya kuchukua maoni ni vijana wenye umri kati ya miaka 15-35 sawa na asilimia 81 ya watu wote waliotoa maoni kuhusu dira hiyo.
0 Comments