Na COSTANTINE MATHIAS, Igunga
SERIKALI kupitia Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), imeendelea kutoa elimu kwa wakulima wa pamba huku ikitambulisha matumizi ya mashine maalum ya kupima unyevunyevu kwenye pamba (Cotton Moisture Meter), kwa lengo la kulinda ubora wa zao hilo muhimu la kibiashara na kudhibiti uchafuzi unaofanywa kwa kuchanganya maji.
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kuboresha sekta ya pamba, kuhakikisha uzalishaji wenye tija na kuongeza thamani ya pamba ya Tanzania katika soko la ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Mkaguzi wa Pamba wilayani Igunga, Benjamini Madama, amesema kuwa mashine hizo zina uwezo wa kupima kiwango halisi cha unyevunyevu kilichopo kwenye pamba na kubaini kama mkulima ameongeza maji kwa makusudi ili kuongeza uzito wa pamba anayopeleka kuuza.
“Pamba inapovunwa shambani huwa na wastani wa unyevunyevu wa kiwango cha 8, endapo mkulima ameichanganya na maji, kipimo hiki huonyesha zaidi ya kiwango hicho, na tunaanza kuwa na wasiwasi wa uchafuzi wa pamba,” amesema Madama.
Ameongeza kuwa hatua kali huchukuliwa kwa mkulima au chama cha msingi (Amcos) kitakachohusika, ikiwa ni pamoja na kutozwa faini au kufikishwa mahakamani.
Aidha, amesema kuwa kupitia Mpango wa Jenga Kesho Bora (BBT), Maafisa Ugani wameongezeka na kusaidia usimamizi thabiti wa ukusanyaji na uuzaji wa pamba kupitia vyama vya msingi.
Maafisa hao pia wamepewa jukumu la kutoa elimu kwa wakulima kuhusu usafi wa pamba na namna bora ya kuvuna ili kuepuka kuchanganya na vikonyo au mchanga.
Katibu Meneja wa Chama cha Msingi Iguna Balimi, wilayani Igunga, Bi. Adelia Nestory, ameipongeza serikali kwa kuleta mashine hizo, akisema zimekuwa msaada mkubwa katika kubaini udanganyifu wa kuchanganya maji kwenye pamba.
Kwa upande wao, wakulima wa vijiji vya Mwajoja wilayani humo wameeleza namna elimu inayotolewa na Maafisa Ugani imechangia kuongeza uzalishaji na ubora wa pamba.
Gamaya Marco amesema zamani wakulima walikuwa wanachuma pamba kwa ukombakomba bila kufuata taratibu sahihi, hali iliyochangia upotevu wa ubora.
“Nimelima ekari tatu na natarajia kuvuna kilo 3000. Uchafu kwenye pamba umepungua sana, na tunaona faida ya juhudi hizi za elimu,” amesema Paulina Mathias, mkulima kutoka kijiji cha Mwajoja.
Licha ya mafanikio hayo, bado changamoto ya baadhi ya wakulima kuvuna pamba ikiwa na vikonyo na mchanga inaendelea kuonekana ambapo Wakulima wameiomba serikali kuongeza usimamizi hasa wakati wa mavuno ili kuhakikisha pamba yote inayokusanywa ni safi na yenye ubora wa hali ya juu.
Kupitia matumizi ya Cotton Moisture Meter, serikali imeonesha dhamira ya kweli ya kulinda ubora wa pamba ya Tanzania, kuhakikisha mkulima anapata bei stahiki na sekta ya kilimo inaendelea kuwa kichocheo cha maendeleo ya uchumi wa taifa.
Mwisho.
0 Comments