Na Matukio Daima Media , Morogoro
Waombolezaji wanaume wawili waliokuwa kwenye basi dogo aina ya Toyota Rosa lenye namba za usajili T.492 EHP wamefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya gari hilo kupinduka na kuangukia korongoni katika kijiji cha Bagilo, kata ya Tegetero, wilayani Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa chanzo chake ni uzembe wa dereva wa basi hilo, Mohamed Sukari, mkazi wa Kimara, jijini Dar es Salaam, ambaye tayari anashikiliwa na polisi kwa mahojiano.
“Dereva huyo alikuwa akiendesha kwa njia za hatari bila kuchukua tahadhari. Uchunguzi wa awali umebaini hakuwa makini kuzingatia jiografia ya eneo husika lenye milima, miteremko na kona kali,” amesema Kamanda Mkama.
Kamanda huyo ameeleza kuwa watu wawili waliopoteza maisha ni wa jinsia ya kiume, huku watano miongoni mwa majeruhi wakikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi. “Tunawashikilia waliohusika ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria,” amesema.
0 Comments