![]() |
Naibu Katibu Mkuu - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Daniel Mushi |
Na. Matukio Daima App, Morogoro
Serikali imewataka walimu wote nchini kuendelea kuwa walezi na kuwasaidia wanafunzi kutojihusisha na tabia zenye kuondoa maadili na utamaduni wa Kitanzania.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Daniel Mushi tarehe 20 Juni 2025 wakati akifungua mafunzo maalumu kwa walimu wa ajira mpya wa masomo ya Elimu ya Bishara na Amali.katika chuo cha Ualimu Morogoro.
“Pamoja na kuwa mnapata mafunzo ya masomo yenu hapa, naomba sana mhakikishe mnapomaliza kupewa ujuzi na nyie muende kuwa wazazi na walezi kwa wanafunzi wetu nchini kwani kumezuka tabia zisizo na maadili” amesema Prof. Mushi.
![]() |
Washiriki |
Prof. Mushi ameendelea kusema kuwa, Serikali imedhamiria kuboresha Sekta ya elimu nchini kwa kuwekeza katika kutoa ajira kwa walimu wapya na kuhakikisha wanapatiwa mafunzo kazini ili kupata uelewa katika kazi hiyo huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa hadhi Sekta ya elimu nchini.
Pia, ameipongeza TET kwa namna inavyoendelea kuratibu mafunzo kwa walimu wote na kuwataka kuhakikisha wanaendelea kuweka moduli zaidi katika mfumo wa kujifunzia walimu (LMS) ili waendelee kujifunza kupitia jumuia zao.
![]() |
Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba |
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuipatia TET fedha katika kutekeleza majukumu yake huku akiongeza kuwa mafunzo haya maalumu yatasaidia sana washiriki kuweza kumudu mbinu mbalimbali zikiwemo za upimaji na tathmini.
Naye, mwakilishi wa washiriki katika mafunzo hayo, Bw Doto Manyanga ameeleza kuwa ni jambo jema wao kupatiwa mafunzo hayo ya muda mrefu ambayo yatawawezesha kufundisha vizuri wanafunzi shuleni na kuendelea kuwa walezi bora.
Mafunzo hayo yanatolewa kwa jumla ya walimu wa ajira mpya 1,699 walioajiriwa kufundisha masomo ya Amali na Elimu ya Biashara kwa shule za sekondari za Serikali Tanzania Bara.
![]() |
Washiriki |
0 Comments