Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima App Dodona
WAKAZI wa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwaletea miradi mikubwa ya maendeleo iliyoboresha maisha yao na kumaliza changamoto nyingi zilizokuwa zikiwakabili kwa muda mrefu.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, yaliyofanyika kwa jina la “Samia Day”, wananchi walisema miradi katika sekta za elimu, afya, maji, barabara, umeme, kilimo, TASAF na utoaji wa mikopo kwa makundi maalum imeleta mafanikio makubwa kwa jamii ya Bahi.
Paskal Mangwela, mkazi wa Kata ya Lamaiti, alisema kata yao imenufaika kwa kiasi kikubwa ambapo zaidi ya shilingi bilioni moja zimetolewa kwa ajili ya miradi ya kimkakati.
“Kupitia TASAF na mikopo ya asilimia 10, wananchi wetu wameweza kuinuka kiuchumi. Kama Lamaiti, hatuna deni kwa Rais wetu – ametufanikishia kila kitu,” alisema kwa furaha.
Kwa upande wake, Juma Hashimu, mkazi wa Kijiji cha Kongogo katika Kata ya Babayu, alisema wamepokea mradi wa ujenzi wa skimu ya umwagiliaji wenye thamani ya Shilingi bilioni 5.6, ambao unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti.
“Pia tumepokea Shilingi bilioni 0.5 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, milioni 100 kwa ajili ya daraja na milioni 30 kwa ujenzi wa maabara ya sekondari. Ni mafanikio ambayo hatukuyatarajia kwa muda mrefu,” aliongeza.
Donald Mejitii, Diwani wa Kata ya Lamaiti, alisema "Samia Day" imekuwa siku mahsusi ya kusherehekea na kutathmini mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Mama Samia.
Alisema miradi ya maji imewezesha vijiji kupata huduma ya maji safi, shule zimeongezewa madarasa na vyoo bora, na wananchi wamewezeshwa kupitia mifugo ya kisasa.
“Tunamuunga mkono Mama Samia kwa moyo mmoja. Kwa kweli ametufanyia makubwa; hatuna deni naye,” alisema Diwani huyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Bw. Johakimu Tobias alisema hafla hiyo imelenga kuonyesha mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, na kueleza mwelekeo wa maendeleo kwa miaka ijayo.
Alisema Wilaya ya Bahi yenye tarafa nne, kata 22, vijiji 59 na vitongoji 552 imenufaika na miradi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 52.6 katika kipindi cha miaka minne.
Alibainisha kuwa fedha hizo zimegusa sekta mbalimbali kama elimu, afya, miundombinu, nishati, na huduma za jamii kwa ujumla.
“Mafanikio haya yamewagusa wananchi wote wa Bahi ni jukumu letu sasa kuilinda amani, mshikamano na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao kwa sababu tuna kila sababu ya kuridhika,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Mwisho
0 Comments