Header Ads Widget

TASAC YAPONGEZWA KWA KUIMARISHA USALAMA WA USAFIRI MJINI.

 



Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima App Dodoma


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, amepongeza juhudi zinazofanywa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) katika kuhakikisha vyombo vya usafiri wa majini vinatoa huduma kwa usalama na ufanisi kwa wananchi.


Waziri Simbachawene alitoa pongezi hizo alipofanya ziara ya kutembelea banda la TASAC kwenye maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma. Alisema hatua zinazochukuliwa na shirika hilo katika kusimamia ubora wa vyombo vya majini ni muhimu kwa maisha ya watu na uchumi wa taifa.


"Ni jambo la kutia moyo kuona taasisi kama TASAC zinachukua hatua za makusudi kuhakikisha usalama wa abiria na mizigo baharini na kwenye maziwa yetu. Nimefurahishwa sana na kazi mliyo nayo," alisema Simbachawene.


Kwa upande wake, Mhandisi Saidi Mkwawa ambaye ni Afisa Msajili na Mkaguzi Mkuu wa Vyombo vya Usafiri Majini kutoka TASAC, alisema shirika hilo limeweka mkazo mkubwa katika ukaguzi wa vyombo vya majini kwa lengo la kudhibiti ubora na kuhakikisha huduma salama kwa watumiaji.


“Tunaendelea kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wamiliki na watengenezaji wa vyombo vya usafiri majini ili kuhakikisha vinajengwa kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa. Pia tunafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maeneo yote ya mwambao na maziwa,” alieleza Mhandisi Mkwawa.


Aidha, Afisa Uhusiano Mwandamizi wa TASAC, Amina Miruko, alieleza kuwa TASAC imeanzishwa kwa mujibu wa sheria ya uwakala wa meli (Sura ya 415), na ilianza rasmi kutekeleza majukumu yake mwaka 2018.


Alisema majukumu hayo ni pamoja na kusimamia sekta ya usafiri wa majini, kuratibu biashara ya usafirishaji wa majini, pamoja na kutoa huduma za uwakala wa meli.


“Kwa sasa tumeimarisha udhibiti wa shughuli zote za usafiri majini ili kulinda maisha ya wananchi, mali zao na pia kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia usafirishaji wa uhakika,” alisema Miruko.


Kwa mujibu wa TASAC, taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha huduma za usafiri majini nchini zinaendeshwa kwa viwango vya hali ya juu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa watoa huduma kuhusu umuhimu wa utii wa sheria na kanuni zilizopo.


Mwisho. 





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI