Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima App Dodoma
Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, alisema kuwa serikali imejipanga kikamilifu kuendelea kulinda haki za watoto na kuhakikisha wanapata huduma bora za malezi, elimu na makuzi salama.
Amesema kuwa mtoto si taifa la kesho pekee bali ni taifa la leo, hivyo ni lazima apewe nafasi ya kukua katika mazingira yanayomjenga kimaadili, kielimu na kiafya.
Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa ikiwemo Mkataba wa Haki za Mtoto, Mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) namba 182 unaolenga kutokomeza aina mbaya za ajira kwa watoto, na mkataba namba 183 unaohusu kazi za wafanyakazi wa majumbani. Licha ya mikataba hiyo, serikali pia inatekeleza Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 ambayo inalinda haki na ustawi wa watoto.
Naibu Waziri Katambi ameeleza kuwa pamoja na kuwepo kwa kazi za staha ambazo mtoto anaweza kushiriki bila kuathiri maendeleo yake, bado kuna idadi kubwa ya watoto walio katika ajira hatarishi hususan kwenye sekta zisizo rasmi.
Amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2014, kiwango cha utumikishwaji wa watoto kilikuwa asilimia 14, na juhudi za serikali zimeendelea kupunguza kiwango hicho kwa kuimarisha ulinzi wa watoto na kutoa elimu kwa jamii.
Katika hatua ya kuimarisha utekelezaji wa sheria na miongozo ya kulinda watoto, serikali imetoa agizo kwa taasisi zote za serikali na sekta binafsi kuhakikisha hazimhusishi mtoto katika ajira ya aina yoyote inayokwenda kinyume na sheria.
"Watoto wengi wanaofanya kazi majumbani na kwenye mashamba hawana ulinzi wa kisheria, na wengi wao wako chini ya miaka 18, jambo linalokiuka haki zao za msingi," Amesema.
Aidha mesema Serikali imesisitiza kuwa watoto wanapaswa kuwa shuleni, wakipata elimu na malezi bora badala ya kufanyishwa kazi zinazowadhalilisha au kuwahatarisha. Wananchi pia wamehimizwa kushiriki katika juhudi za kuwalinda watoto kwa kutoa taarifa pale wanapobaini matukio ya ajira haramu kwa watoto katika jamii zao.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Groly Emmanuel, alisema kuwa zaidi ya watoto milioni 160 duniani wanatumikishwa, huku wengi wakijihusisha na kazi hatarishi, hasa katika kilimo.
“Mtoto wa kike bado anaathirika zaidi, hasa katika ajira za ndani ambazo mara nyingi hufanyika kwa siri na bila ulinzi wa kisheria,” amesema Emmanuel.
Na kuongeza Ameongeza kuwa asilimia 24.9 ya watoto hao wanahusika na kazi mbaya zaidi kama migodini, usafirishaji haramu na unyanyasaji wa aina mbalimbali.
Emmanuel ametoa wito kwa nchi wanachama wa ILO kuwekeza zaidi kwenye ajira zenye staha kwa wazazi, kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii na kutoa elimu kwa jamii kuhusu athari za ajira kwa watoto ili kuondoa utegemezi wa kipato kutoka kwao.
Naye Kamishna wa Kazi, Susan K. Mkangwa, amesema Serikali kupitia Idara ya Kazi imeanza maandalizi ya kaguzi maalum katika mashamba, migodini na maeneo ya kazi ili kubaini watoto wanaotumikishwa na kuwachukulia hatua waajiri wote wanaohusika.
“Tutazindua kampeni za kitaifa za uelimishaji ili kuifikia jamii moja kwa moja. Lengo letu ni kuhakikisha hakuna mtoto anayepoteza haki yake ya elimu na utoto kwa sababu ya tamaa ya kipato cha haraka,” amesema Kamishna Mkangwa.
0 Comments