Header Ads Widget

SERIKALI YADHAMIRIA KUPUNGUZA MATUMIZI YA KUNI NA MKAA

 


 Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App Dodoma

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Mpango amesema Serikali imeweka dhamira ya dhati kupunguza athari za uharibifu wa mazingira kwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa kwa shughuli za kupikia katika taasisi zinazohudumia watu wengi

Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma Dkt Mpango alisema Serikali tayari imepiga marufuku matumizi ya kuni na mkaa katika taasisi zinazopika kwa watu zaidi ya mia moja kwa siku na kuzitaka zitumie nishati safi ya kupikia.


Alibainisha kuwa kufikia Machi 2025 jumla ya taasisi 762 zitakuwa zimeanza kutumia nishati safi ambapo kati ya hizo taasisi za umma ni 495 na taasisi binafsi ni 267

Makamu wa Rais ametoa wito kwa wadau wa mazingira kuendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia za urejelezaji wa taka na plastiki kupunguza ukataji miti ovyo na kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia

Amesisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi za upandaji miti na uanzishaji wa bustani za kijani akisema jukumu la kulinda mazingira linahitaji ushirikiano wa wadau katika ngazi zote

Aidha Dkt Mpango amesema ripoti mbalimbali za mazingira zinaonyesha kuwa karibu asilimia 61 ya ardhi nchini iko katika hatari ya kuharibika kutokana na shughuli za kibinadamu zisizo endelevu zikiwemo ongezeko la mifugo isiyolingana na uwezo wa ardhi ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa kilimo cha kuhamahama uchimbaji holela wa madini na upanuzi wa makazi usiozingatia mipango miji.

Amesema Serikali imechukua hatua kadhaa kukabiliana na hali hiyo ikiwemo kupitishwa kwa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 na Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira kwa miaka kumi kuanzia 2022 hadi 2032.


Hatua nyingine ni pamoja na kuhamasisha matumizi endelevu ya ardhi kwa njia za kilimo mseto kilimo cha matuta kilimo hifadhi na mbinu za asili za hifadhi ya malisho pamoja na kuongeza kasi ya upimaji na umilikishaji wa ardhi.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Rais Wabunge na Madiwani kwa kugombea kushiriki kwenye kampeni na kujitokeza kwa wingi kupiga kura huku akiwataka kudumisha utulivu na amani katika kipindi chote cha uchaguzi hadi baada ya matokeo kutangazwa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Khamis Hamza Khamis amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inahimiza jamii kupunguza matumizi ya bidhaa za plastiki kwa kukuza uzalishaji na matumizi endelevu ili kulinda mito maziwa na bahari kwa ajili ya kuhifadhi mifumo ya ikolojia.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo Tuwajibike Sasa Dhibiti Matumizi ya Plastiki.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI