Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza amefanya ziara katika kata za Ilembo na Santilya ambapo pamoja na kutekeleza miradi mbalimbali pia amekagua barabara ya Ilembo Sapanda inayojengwa kwa zaidi ya shilingi billion moja na million mia mbili.
Kwa mujibu wa wataalam (TARURA) wilayani Mbeya barabara ya Ilembo Mwala Sapanda imeanza kujengwa Juni 2025 na inatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 2025.
Kwa niaba ya Meneja wa Wakala wa barabara za mjini na vijijini TARURA wilayani Mbeya Mhandisi wa TARURA wilaya ya Mbeya Geofrey Magila, amesema mpango uliopo ni kujenga barabara ya Ilembo Mbagala yenye urefu wa kilomita 5.2 ikiwemo daraja la Iwonde na maombi ya wananchi ni kuona barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha kifusi.
Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza, amesema kazi ya kiongozi yeyote ni kusaidia kuwaletea maendeleo wananchi wake na kuwataka wananchi kutosikiliza maneno ya viongozi waongo akisema ni sumu ya maendeleo.
Pamoja na mambo mengine mbalimbali Mbunge huyo amekabidhi mchango wake wa shilingi million tatu kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za wananchi wa Kijiji cha Mwakasita kata ya Ilembo kwenye ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ambavyo vipo kwenye hatua ya umaliziaji huku mchango mwingine ukitarajiwa kutoka Halmashauri ya wilaya ya Mbeya ili kuboresha shule hiyo.
Kaimu afisa elimu msingi na sekondari wilaya ya Mbeya Mwalimu Fabian Mtisi amempongeza Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini kwa kuendelea kupigania maendeleo ya wananchi wake ikiwemo kwenye sekta ya elimu ambapo amesema Halmashauri imeendelea kutoa fedha kwenye miradi mbalimbali ya elimu ikiwemo katika kijiji cha Mwakasita na kata ya Ilembo.
0 Comments