Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
MBUNGE wa Jimbo la Bariadi, Mhandisi Kundo amewataka wananchi wa Kata ya Guduwi, Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu kumpigia kura za Kishindo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu ili aendelee kutekeleza miradi ya Maendeleo.
Mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji amewataka wananchi hao kumweshimisha Rais Dkt. Samia kutokana na uchapakazi wake uliojidhihirisha kutokana na Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mhandisi Kundo ameyasema hayo jana kwenye mkutano wa kuwasilisha Utekelezaji wa Ilani ya CCM (2020/2025) katika kata ya Guduwi na kueleza kuwa kata hiyo ilipokea kiasi cha Shilingi Mil.287. 6 za miradi ya Maendeleo kwa miaka mitano ( 2015/2020) lakini kipindi cha miaka mitano ya Rais Dkt. Samia kata imepokea shilingi bil.1.366 (2020/2025).
Ameongeza kuwa atahakikisha anawasilisha mahitaji ya wananchi hasa ujenzi wa daraja la mto Bariadi linalounganisha na kufungua mawasiliano baina ya Tarafa ya Ntuzu na kata ya Guduwi.
"Oktoba mwaka huu, twendeni tukamuheshimishe Rais Samia Suluhu kwa kumpa kura za kishindo sababu ameleta Mradi kutoka Ziwa Victoria na tutahikisha Guduwi inafunguka kwenye mawasiliano hasa barabara kwa kujenga Daraja kwenye mto Bariadi" amesema.
Kuhusu kuendeleza sekta ya michezo, Mhandisi Kundo amekabidhi Mipira 35 kwa ajili ya Mitaa 8 ya kata hiyo pamoja na jezi pea 9, ambapo kila mtaa umepewa jezi pea moja, mipira minne huku Kata ya Guduwi ikikabidhiwa jezi pea moja na mipira 3.
Mwisho.
0 Comments